RAIS wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Kikwete na Waziri wa Misaada ya Kimataifa ya Maendeleo wa Uingereza, Mheshimiwa Andrew Mitchel wamezungumza kuhusu fedha ambazo Tanzania inadai ilipwe na kampuni ya kuuza silaha ya nchini British Aerospace (BAE).
Katika mazungumzo hayo kwenye Ukumbi wa Palace of Conferences katika kijiji cha Sipopo, nje kidogo ya mji mkuu wa Equatorial Guinea katika Kisiwa cha Bioko, viongozi hao wawili wamekubaliana kuendelea na jitihada za kuishawishi BAE kuilipa Tanzania fedha hizo ambazo ni haki yake.
Tanzania inadai kulipwa fedha zake kiasi cha paundi za Uingereza milioni 29.5 zinazotokana na Tanzania kutozwa kiasi kikubwa zaidi kuliko kile kilichotakiwa kulipwa wakati inanunua rada kutoka BAE.
Ununuzi wa rada hiyo ulisababisha matatizo makubwa yakiwemo madai ya rushwa na hatimaye kampuni hiyo ya BAE ilifikishwa mahakamani kwa madai hayo ya kutoa rushwa katika ununuzi wa rada hiyo.
Hatimaye mahakama iliamua kuwa BAE haikutoa rushwa isipokuwa kuwa ilifanya makosa katika vitabu vyake vya mahesabu lakini kampuni ikaamuliwa pia kulipa kiasi cha paundi milioni 29.5 kuirudishia Tanzania ambayo ni fedha yake kihalali kwa sababu ilidhulumiwa fedha zake.
Hata hivyo, kampuni hiyo pamoja na kuamuliwa kuilipa Tanzania moja kwa moja, iliamua kutoa fedha hizo kwa taasisi isiyokuwa ya kiserikali ambayo ndiyo ingeleta fedha hizo Tanzania kwa njia ya kutoa huduma.
Tanzania imepiga hatua hiyo na majuzi ilitoa taarifa kali Bungeni kupinga hatua hiyo ya BEA, Serikali inataka kuziingiza fedha hizo katika kuboresha elimu ikiwa ni pamoja na kununua vitabu kwa ajili ya wanafunzi na kujenga madarasa na nyumba za walimu.
Viongozi hao wawili pia wamezungumzia hali ilivyo katika Libya ambako Rais Kikwete amemwelezea Mheshimiwa Mitchel maoni ya viongozi wa waafrika kuhusu kampeni ya kuipiga mabomu inayoendeshwa na majeshi la Umoja wa Kujihami wa Ulaya (NATO) dhidi ya Libya.
Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini,
Malabo, Equatorial Guinea.
01 Julai, 2011