RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameishukuru Marekani na Shirika lake la Misaada la Millenium Challenge Corporation – MCC- kwa msaada wa mabilioni ya fedha ambao umechangia kuboresha miundombinu nchini na kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha, Rais Kikwete amelishukuru taifa hilo kubwa na MCC kwa uamuzi wake wa kutoa awamu ya pili ya msaada kama huo kwa Tanzania ambao maandalizi yake yameanza. Rais Kikwete ametoa pongezi hizo leo, Aprili 8, 2013 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa MCC, Bwana Daniel Yoannes Ikulu, mjini Dar es Salaam.
Yoannes yuko nchini kuzindua baadhi ya miradi iliyogharimiwa na msaada wa dola za Marekani milioni 689 ambao Serikali ya Tanzania imeutumia katika kujenga ama kuboresha miundombinu ya barabara, umeme, viwanja vya ndege na maji.
Miongoni mwa miradi ambayo itazinduliwa kwa pamoja na Rais Kikwete na Bwana Yoannes wakati wa ziara yake katika Tanzania ni ujenzi wa barabara ya Tanga-Horohoro kwa kiwango cha lami, njia ya kulaza nyaya za kusafirishia umeme chini ya Bahari ya Hindi kutoka Bara hadi Zanzibar, na njia ya kusafirisha umeme na kuusambaza katika wilaya mbali mbali nchini kutokea Mkoani Dodoma.
Hiyo ni baadhi ya miradi michache kati ya mingi inayogharimiwa na msaada huo ambayo tayari imekamilika tayari kuzinduliwa. Mingine mingi inaendelea kujengwa.
“Msaada wenu umetuwezesha kufanya mambo makubwa kama vile kujenga barabara katika maeneo ambako hakuna mshirika mwingine yoyote wa maendeleo alikuwa tayari kutusaidia, na sisi wenyewe tulikuwa hatujapata uwezo wa kiraslimali wa kujenga barabara hizo,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Baadhi ya barabara hizo ni ule ya Tunduma-Sumbawanga na Namtumbo-Songea. Kuna kiongozi wa nchi moja ambaye nilimpata kumwomba msaada wa kuijenga barabara hii na akasema kuwa ilikuwa vigumu kwa nchi yake kujenga barabara inatoka kusikojulikana kwenda kusikojulikana. Nawashukuru nyie kwa msaada wenu mkubwa.”
MCC ilitangaza kuipa Tanzania msaada huo wa mabilioni ya fedha Desemba 2005.