Na Mwandishi Maalum
RAIS Jakaya Kikwete ameahidi kuwa Serikali yake ipo tayari kutekeleza mapendekezo juu ya namna ya kuboresha utawala bora kama yatakavyotolewa na wataalamu wa Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
Rais Kikwete aliyasema hayo juzi jioni alipokuwa akiagana na timu ya wataalamu kutoka makao makuu ya APRM waliokuwa nchini kwa takribani wiki tatu kuhakiki ripoti ya ndani ya nchi kuhusu utawala bora iliyokuwa imeandaliwa na wataalamu wa APRM Tanzania.
Katika wiki tatu walizokuwa hapa nchini wataalamu hao wakiongozwa na Wakili mashuhuri nchini Cameroun, Akere Muna aliyeambatana na wataalamu wengine mabingwa barani Afrika kama Profesa Abdul Aziz Jalloh, Prof. Ahmed Muhiddin na mmoja wa washauri wa aliyekuwa Rais wa Zambia, Rupiah Banda, Dk. Francis Chigunta, walikutana na wadau mbalimbali wa masuala ya utawala wakiwemo viongozi wa Serikali na wadau wa sekta binafsi.
“Nawapongeza kwa moyo wenu wa dhati wa kutusaidia kutathmini hali ya utawala bora katika nchi yetu. Sisi tulijitazama wenyewe kwa kujitathmini kwa kutumia taasisi yetu ya APRM Tanzania. Ujio wenu ni muhimu kwa sababu sasa mtatueleza wapi tunafanya vizuri tuimarishe na wapi tunakosea turekebishe.
“Serikali yangu itayasubiri kwa hamu mapendekezo yenu ili nasi tuwapatie majibu ya nini tumefanya. Lakini la muhimu zaidi ni kwamba tunaahidi kuyafanyiakazi mapendekezo yenu kwa faida ya nchi yetu,” alisema Rais Kikwete.
Awali akimweleza Rais jinsi mchakato huo wa uhakiki ulivyofanyika nchini, Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib alisema katika kipindi cha wiki tatu walizokuwa nchini, wataalamu hao walifanya mikutano na wadau katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Arusha, Dodoma, Mbeya, Mtwara, Ruvuma, Unguja na Pemba ambapo takriban wadau 1,300 walifikiwa na wakatoa maoni yao.
Aliongeza kuwa mbali ya wadau hao pia wataalamu hao walifanikiwa kukutana na makundi maalum kama vile wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, Spika wa Bunge, majaji, watendaji wakuu wa taasisi za biashara, makatibu wakuu wa wizara na viongozi waandamizi wa Serikali akiemo Rais Kikwete mwenyewe, Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad na Makamu wa Pili, Balozi Ali Seif Iddi.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usimamizi la APRM, Prof. Hasa Mlawa alimweleza Rais Kikwete kuwa katika awamu hii ya utekelezaji wa shughuli za APRM yeye na watendaji wenzake wamejifunza mambo mengi ikiwemo haja ya Serikali kuongeza elimu ya uraia kwa watu wake ili wawe wazalendo zaidi na pia kuiimarisha taasisi ya APRM hapa nchini.
“Kwa kuzingatia pia umuhimu wa taasisi hii ya APRM katika kukutanisha wadau na Serikali yao, ni vyema pia APRM ikawezeshwa zaidi kwa vifaa, raslimali watu na mafunzo ili kuijengea uwezo wa kitaasisi hususani katika kazi zijazo za kusimamia Mpango Kazi wa Kitaifa wa namna ya kuondoa changamoto zilizoelezwa na wananchi kupitia ripoti hiyo,” alisema Prof. Mlawa.