RAIS Jakaya Kikwete amesema atalisimamia suala la maji koani Mtwara hadi kuhakikisha shida ya maji inakoma mkoani humo. Rais Kikwete amesema hayo wilayani Newala ambapo yuko kwa ajili ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagua na kukichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuongoza tena Tanzania na pia kufuatilia utekelezaji wa ahadi alizotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita.
“Kilio kikubwa mkoani hapa ilikuwa maji na mkulima wa korosho kupata bei isiyo ya uhakika”. Rais amekumbushia na kueleza utekelezaji wa ahadi hizo ulipofikia.
“Tutalimaliza tatizo la maji, kwa bahati nzuri maji yapo ya kutosha chini ya ardhi, suala ni kuyafikisha kwa watu”. Rais amewahakikishia wananchi wa Newala wakati anatembelea mradi wa maji wa Kitangari na baadae katika mkutano wa hadhari kijijini hapo.
Rais amesema serikali itatenga maji ya kutosha kwa ajili ya kuyasambaza maji hayo kwa wananchi. Kuhusu zao la Korosho ambalo ndiyo chanzo kikubwa cha mapato katika mkoa wa Mtwara Rais amesema serikali imeshalipia madeni vyama vya ushirika nchini kuviwezesha kukopesheka na pia utaratibu mpya ulioanzishwa wa stakabadhi ghalani ni njia moja wapo inayowasaidia wananchi kuwa na uhakika wa soko na bei ya korosho yao.
Rais amesema serikali itaendelea kuusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa lengo la kuuimarisha zaidi na hatimaye wananchi wafikie hatua ya kuuza korosho yao ikiwa imebanguliwa
Tayari baadhi ya wakulima wameanza kuuza korosho iliyobanguliwa ambayo inaongeza thamani ya zao hilo.
Rais amefungua ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kuweka jiwe la msingi katika kituo cha Polisi, ofisi hizi mbili zilikua zinatumia majengo ya zamani.
Rais alipata fursa ya kutembelea Kikundi cha Wakulima cha Kitama ambacho kinajihusisha na ubanguaji wa korosho, ambacho kimeanza kazi miaka mitano (5) iliyopita.
Rais amewaeleza wana kikundi nia ya serikali yakusaidia jitihada hizo za wakulima katika vikundi vyao ili waweze kuongeza ubora na thamani ya korosho zao na hatimaye kuongeza kipato chao.
Rais pia ametembelea kiwanda cha River Valey Food na kuweka jiwe la msingi katika ghala la Tandahimba, Newala Co-operative Union (TANECU) ambapo Rais amesisitiza utunzaji wa mapato katika vyama vya ushirika kwani ndiyo chombo pekee kinachoweza kumkomboa mkulima. Rais leo (28 Julai, 2011) anatembelea wilaya za Masasi na Nanyumbu.