Kikundi cha Maduma na mafanikio ya miche

Na Mwandishi Wetu, Muheza

UNAPO zungumzia kati ya vikundi vilivyofanikiwa katika ufanyaji wa shughuli zake wilayani Muheza ni vigumu kutokitaja kikundi cha miche ya machungwa cha Maduma. Kikundi hiki ambacho kipo kijijini Maduma ni wazalishaji na wauzaji wa miche wenye mafanikio makubwa.

Kikundi kilianzishwa mwaka 2003 kikiwa na wanachama watano yaani wanaume wawili na wanawake watatu. Kwa sasa kikundi kina wanachama 12, wanaume saba na wanawake watano.

Kikundi kina ekari sita na mpaka sasa ekari tatu kati ya hizo zimeshapandwa miche ya michungwa huku wakiwa na uhakika wa kuzalisha hadi miche 50,000 kwa msimu. Kikundi kinazalisha miche bora ya machungwa aina ya Late Valencia, Early Valencia (Msasa), Delta Valencia na Washington navel (isiyokuwa na mbegu).

Mti mama unaotumika kuungia miche hii ni milimao ya kawaida. Kikundi hiki kinauza miche tangu kuanzishwa kwa kitalu hiki na mwenyekiti wa kitalu hiki, Fredrick Chapumba anakiri kuongezeka kwa soko baada ya mradi wa MUVI kukitangaza kikundi hiki kwa njia ya vijarida, kama anavyooeleza hapa chini.

“Mwaka 2007/2008 kikundi kiliuza miche 7800 yenye thamani ya Tshs. 3,120,000, Mwaka 2008/2009 kikundi kiliuza miche 11,500 yenye thamani ya sh. 5,750,000, mwaka 2009/2010 kikundi kiliuza miche 16,000 yenye thamani ya sh. 8,000,000 na Mwaka 2010/2011 kikundi kiliuza miche 10,200 bora ya machungwa yenye thamani ya sh. 8,160,000”

Kikundi kimepata elimu ya uzalishaji miche bora ya michungwa, mafunzo ya kilimo cha kibiashara, ujuzi, Ujasiriamali na usimamizi wa biashara yote hayo yametolewa na Mradi wa MUVI kupitia maafiasa ugani. Pia mradi wa MUVI umetusaidia kupata miche bora ya michungwa yasiyokuwa na mbegu Delta Valencia na kupanda katika mashamba ya wanakikundi, kuongezeka kwa kipato cha kaya.

mwaka 2011 kikundi kilipata mkopo wa sh. 1,800,000 kutoka SIDO kwa kuunganishwa na Mradi wa MUVI. Fedha hizi zimetumika katika kuongeza uzalishaji wa miche bora na kununua miundombinu ya kumeagilia bustani ya miche (Pampu na mipira)