Na. Aron Msigwa.
KIKAO kazi cha Maafisa habari wa Serikali kutoka Wizara, taasisi, wakala wa serikali, mashirika ya umma, mikoa na wilaya mbalimbali nchini leo kimeingia siku ya pili mjini Dodoma kwa maafisa hao kupata fursa ya kujadili changamoto zinazokabili vitengo vya habari na mawasiliano serikalini na namna ya kuzitatua.
Katika kikao hicho mada mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo ile ya Mwongozo wa Ofisi za Mawasiliano serikalini iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Msaidizi kutoka Idara ya Habari (MAELEZO) anayeshughulikia uratibu wa vitengo vya mawasiliano serikalini akitoa msisitizo mkubwa kwa maafisa habari kuyafahamu vizuri majukumu yao ya kazi kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma ili kuboresha utendaji wa kazi.
Pia maafisa hao wamepata fursa ya kujifunza namna ya kuboresha mawasiliano serikalini kupitia mada ya mkakati wa mawasiliano (Communication Strategy) wa kuiwezesha jamii kupata taarifa sahihi kwa muda muafaka ,mada iliyowasilishwa na Meneja mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Innocent Mungy.
Katika mada hiyo Bw. Mungy ametoa wito kwa maafisa hao kuzitumia nafasi zao kutoa taarifa kwa umma mara kwa mara ili kuwapa fursa wananchi kufahamu yale yanayofanywa na serikalini.
Ametoa wito maafisa hao kushirikiana na vyombo mbalimbali vya habari katika kutekeleza mkakati huo kwa kuhakikisha kuwa wanatoa habari kwa umma kupitia radio, magazeti, televisheni na mitandao ya kijamii ili kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa na jamii kukosa taarifa sahihi za serikali za utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.