Kijana Edmund Rutaraka Ajitosa Ubunge Moshi Mjini

Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na Naibu Kamanda wa Vijana CCM, Manispaa ya Moshi, Edmund Rutaraka.

Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na Naibu Kamanda wa Vijana CCM, Manispaa ya Moshi, Edmund Rutaraka.

Na Dixon Busagaga

SIKU chache baada ya kumalizika mchakato wa kumpata kada atakaye peperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kinyang’anyiro cha kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makada wa chama hicho sasa wamerejea majimboni na kuanza harakati za kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea Ubunge.

Hali hiyo inajitokeza katika Jimbo la Moshi mjini, baada ya vijana wa chama hicho kuonekana kuhamasika huku wakijitokeza kutangaza nia ya kuwania nafasi ya Ubunge na kutishia harakati za baadhi ya makada wakongwe ndani ya chama hicho.

Waliojitokeza na kutangaza nia hadharani hadi sasa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na Naibu Kamanda wa Vijana CCM, Manispaa ya Moshi, Edmund Rutaraka (37) na Mwenezi wa Chama hicho wilaya ya Moshi mjini Priscus Tarimo, diwani wa kata ya Kilimanjaro aliyemaliza muda wake.

Rutaraka ambaye ni msomi mwenye Shahada ya Uzamili, (M.BA) ya Chuo cha Uongozi, Esami na Shahada ya Sayansi ya Chakula na teknolojia ya Chuo kikuu cha Sokoine (SUA), alisema CCM katika jimbo la Moshi
mjini kwa sasa kinapaswa kumsimaisha mtu mwenye hekima, Busara na Mcha Mungu.

“Kiongozi kwa sasa atakaye tosha kupeperusha chama chetu ni yule atakaye weza kusimamia vema rasirimali zilizopo katika jimbo letu na si yule mwenye maneno ya kulaghai wananchi”alisema Rurataka.

Rutaraka ambaye pia ni mjumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi alisema baada ya kushauriwa na wazee, kujitathmini na kupima uwezo wake ameona anatosha kuwawakilisha wananchi wa jimbo la Moshi mjini.

“Nimeshauriwa na wazee, nikajitathimini na kupima nikaona kwamba ninatosha kuwa mwakilishi mwema wa wananchi wa jimbo la Moshi mjini hivyo basi naomba nitumie muda huu kutangaza rasmi nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Moshi mjini,” alisema Rutaraka ambaye pia ni naibu kamanda wa vijana wa CCM
manispaa ya Moshi.

Alisema kwa namna hali ilivyo sasa chama Cha Mapinduzi kinapaswa kuwa na viongozi vijana ambao wataweza kuliongoza taifa kwa ujumla, kwani vijana ndio wenye nguvu na ambao wanaweza kuleta mabadiliko kwa haraka zaidi. Rutaraka alisema kama kijana ameamua kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo la Moshi mjini ili kulikomboa kutoka Upinzania na kurudi Chama cha Mapinduzi huku akiwaomba vijana wenzake kumuunga mkono.

“Kazi ya mbunge ni kuisimamia na kuishauri serikali hivyo basi uwezi kufanya hivyo kama huna dhamira ya kweli ya kuingia kwenye bunge kwa ajili ya kufanya kazi ya wananchi,” alisema Rutaraka

Kuhusu vipaumbele vyake Rutaraka alisema ni kuhakikisha huduma za afya zinapewa nafasi ya kwanza hasa kwa Mama wajawazito na watoto na kwamba huduma muhimu hazikosekani katika Hospitali, Zahanati na vituo vya Afya vilivyoko ndani ya jimbo la Moshi mjini. Mbali na kipaumbele hicho Rutaraka pia alisema atahakikisha anawatetea walemavu wa aina zote ikiwa ni pamoja na kusaidia angalau wanapata nafasi ya kufanya kazi ambazo wanauwezo nazo.

Pia alisema atahakikisha anasimamia miundo mbinu na kusaidia watu wanapata hati za viwanja vyao kwani kuna baadhi ya kata wananchi wanashida ya ardhi na viwanja havijapimwa katika manispaa.

Kujitokeza kundi hilo la vijana kunafanya idadi ya makada wa chama hicho walioonesha nia ya kutaka kugombea Ubunge katika jimbo hilo lililoomgozwa na Philemoni Ndesamburo (Chadema) kufikia 12 hadi sasa licha ya uwepo wa baadhi yao kungojea kukamilika kwa mkutano mkuu wa Chama hicho mjini Dodoma.