Kifungo dereva ajali ya Chacha Wangwe batili

Aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Marehemu Chacha Wangwe

Uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma wa kumhukumu kifungo cha miaka mitatu jela, dereva Deus Mallya aliyekuwa anamwendesha aliyekuwa Mbunge wa Tarime (Chadema), marehemu Zakayo Chacha Wangwe, umetenguliwa na Mahakama ya Rufani.

Mallya alihukumiwa Machi 18 mwaka 2008 na aliyekuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, Thomas Simba.

Mallya, ambaye uhusiano wake na marehemu Wangwe ulizua mjadala miongoni mwa wanasiasa na jamii kwa ujumla, baada ya kutokea ajali hiyo, alihukumiwa kifungo hicho baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili.

Kosa la kwanza lilikuwa ni kuendesha gari kwa mwendo kasi na kusababisha ajali, iliyomuua Wangwe na kosa la pili ni kuendesha gari bila leseni.

Wangwe, ambaye wakati anafariki dunia alikuwa amesimamishwa wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, alifariki dunia katika ajali hiyo iliyotokea eneo la Pandambili, Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma Julai 28, 2008 saa 2:55 usiku akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda jijini Dar es Salaam.

Baada ya kutolewa hukumu hiyo, Mallya alikata rufaa mwaka 2010, ambayo ilisikilizwa na Jaji Mwanaisha Kwariko wa Mahakama Kuu ya Kanda ya Dodoma.

Hata hivyo, Jaji Mwariko katika hukumu yake alisema kuwa Mallya anapaswa kuendelea na adhabu hiyo ya kuitumikia adhabu hiyo jela kwa miaka mitatu.

Kikao cha jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa Kanda ya Kati Dodoma, juzi kilitengua maamuzi yote yaliyotolewa awali na Mahakama ya Wilaya ya Dodoma na Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma dhidi ya Mallya (27).

Akisoma uamuzi wa jopo la majaji hao juzi, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa Kanda ya Kati, Maxmillian Malewo, alisema kuwa uamuzi wa kutengua maamuzi ya awali ulitolewa na jopo la majaji wa tatu wakiongozwa na Jaji Harold Nsekela.

Malewo alisema maamuzi hayo yametokana na sababu kuu mbili, ambazo ni kesi kufunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini badala ya Mahakama ya Wilaya ya Kongwa ambako tukio hilo lilipotokea.

Sababu nyingine ni kesi hiyo ambayo ni ya usalama barabarani ilitakiwa kufunguliwa katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma na si Mahakama ya Wilaya ya Dodoma.

Alisema kikao hicho pia kilionya kesi hiyo kutokutumika kama kesi ya mfano katika kesi nyingine zitakazotokea kutokana na kusikilizwa kimakosa na kutoa hukumu kimakosa.

CHANZO: NIPASHE