RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kufadhaishwa na taarifa za kifo cha Mjumbe waTume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi kilichotokea, Novemba 12, 2013 kwenye Hospitali ya Milpark, Johannesburg, AfrikaKusini.
Katika salamu za rambirambi ambazo amemtumia Mwenyekitiwa Tume hiyo, Jaji Joseph SindeWarioba, Rais Kikwete amesema kuwa amepokea kwa mshtuko mkubwa na fadhaha taarifa za kifo cha Dk. Mvungi. “Kwa hakika ni taarifa iliyonisumbua na kunipa huzuni nyingi.”
Rais Kikwete amesema kuwa hakuna shaka kuwa katika maisha yakeDk. Mvungi ametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa namna mbalimbali na kuwa kifo kimemfika wakati Taifa la Tanzania lilikuwa bado linahitaji busara, hekima na mchango wake katika mchakato mzima wa kusaka Katiba mpya.
“Kuanzia alipokuwa mwandishi wa habari katika Magazeti ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Uhuru na Mzalendo, hadi uhadhiri wake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hadi uwakili katika Kampuni ya South Law Chambers, hadi uongozi wake katika Chama cha NCCR-Mageuzi, hadi uamuzi wake wa kugombea Urais wa Tanzania mwaka 2005 na sasa akiwa Mjumbe wa Tume ya Katiba, Dk. Mvungi ametoa mchango wake mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu. Na hili hatutalisahau,” amesema Rais Kikwete.
“Kwa masikitiko makubwa, nakutumia wewe Jaji Joseph Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu nikiombeleza kifo cha Dkt. Mvungi. Nakupa pole nyingi wewe Mwenyekiti, wajumbe wa Tume na wafanyakazi wote wa Tume kwa kuondokewa na mwenzenu. Naungana nanyi kuombleza msibahuo mkubwa.”
“Aidha, kupitia kwako, natuma pole nyingi kwa wana-familia, ndugu, marafiki nan majirani wa Dk. Mvungi kwa kuondokewa na mhimili,msimamizi wafamilia na ndugu. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa.Wajulishe kuwa msiba wao ni msiba wangu pia. Muhimu waelewe kuwa binafsi naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu na namwomba Mwenyezi Mungu awape subira waweze kuvuka kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi yake.”
Amemalizia Rais Kikwete: “Napenda kuungana nao katika kumwomba MwenyeziMungu, Mwingi wa Rehema, aiweke mahali pema roho ya Marehemu Dk. Sengondo Mvungi. Amina.”
Wakati huo huo Rais Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Marehemu Musa Hillal Samizi ambaye alifariki tarehe 11 Novemba, 2013 hapa Dar es Salaam. Rais amemwelezea marehemu Samizi kama kada mahiri na mtumishi mwaminifu katika uhai wake.
Rais amesema “Marehemu Samizi atakumbukwa kwa upendo, ushirikiano na uchapakazi wake katika kazi na katika nafasi mbalimbali ambazo aliwahi kushika ndani ya Chama cha Mapinduzi na Serikalini”.
Marehemu Samizi aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Katibu Msaidizi wa Chama cha Mapinduzi Makao Makuu Dodoma, Afisa Utumishi NBC, Mjumbe wa NEC, Mjumbe wa Bodi MECCO, SHIHATA, Serengeti Safari Lodge pamoja na Mkuu wa Wilaya za Handeni, Kasulu, Tabora na Moshi kabla ya kustaafu Mwaka 2012 alipostaafu.
Wakati huo huo; Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Abdulrahaman Kinana amesikitishwa na taarifa ya kifo Cha Dk. Sengondo Mvungi kilichotokea Jana katika Hospitali ya Millpark nchini Afrika ya Kusini. “Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi, Katibu Mkuu anawapa pole wanafamilia, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba na Uongozi wa Chama Cha NCCR-Mageuzi. Hakika Taifa limepoteza Mtaalamu wa Sheria, Kiongozi Mzalendo na hodari katika kipindi ambacho mawazo yake yanahitajika kwa kiasi kikubwa kuliendeleza Taifa hili.” ilisema taarifa ya CCM iliyosaidiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi.
Mungu ilaze mahali pema Roho ya marehemu Samizi. Amen.