Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani imeahidi kuwalipa wananchi wanaostahili kulipwa fidia ya ardhi ambayo ilichukuliwa na Serikali kwa lengo la kutekeleza mradi wa kitovu cha Mji wa Kibaha (CBG) unaotegemewa kujengwa katika eneo la Machinjioni.
Akizungumza kuhusiana na madai ya wananchi wa eneo la Machinjioni Mjini Kibaha, Afisa Habari wa Halmashauri ya Mji huo Innocent Byarugaba amesema Halmashauri hiyo ipo katika maandalizi ya kuitisha kikao na wananchi wa eneo la Machinjioni ili kufanya tathmini ya wanaostahili kulipwa na kuanza utaratibu wa kuwalipa.
Amefafanua kuwa zoezi la kufanya tathmini katika eneo hilo lilishindikana kutokana na wafanya tathmini kufanyiwa fujo hivyo kukwamisha utekelezaji wa zoezi hilo kwa wakati.
“ Kabla eneo hili la Machinjioni halijabadilishwa matumizi kutoka kuwa eneo la viwanda na kubadilisha kuwa eneo la mradi wa kitovu cha Mji wa kibaha (CBG), Halmashauri haikuwahi kutoa kibali kwa mwananchi yoyote kuendeleza eneo hilo na wale wanaodai kuwa eneo hilo ni lao ni wavamizi na Halmashauri inafanya ustarabu tu kuwalipa wale walioendeleza ili kuondoa malumbano yaliyopo”Alisema Byarugaba.
Aidha Halmashauri ya inaendelea kupima eneo la Machinjioni kwa hilo kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi ili kupisha utekelezaji wa mradi huo.
Innocent Byarugabana amewaasa wakazi wa Mji wa Kibaha kutovamia maeneo na kuyaendeleza bila kuwa na hati ya umiliki wa eneo husika.
Halmashauri ya Mji wa Kibaha ipo katika mikakati ya kuendeleza maeneo ambayo yapo katika mikakati ya kufanyiwa miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kuhakikisha Sheria no 2007 ya uendelezaji wa Miji ya mwaka 2008 inatekelezwa.