Muda wa kumalizika kwa kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama iliyofunguliwa na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, na wenzake 10 dhidi ya Chama Cha Wananchi (CUF), umesogezwa mbele, tofauti na makubaliano ya awali yaliyofikiwa baina ya pande mbili hizo.
Makubaliano hayo yalifikiwa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Augustine Shangwa, kwamba kesi hiyo iwe imemalizika ifikapo Machi 13. Lakini jana Jaji Shangwa aliisogeza mbele kesi hiyo hadi Aprili 3, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa.
Uamuzi huo ulifikiwa na Jaji Shangwa baada ya kukubaliana na hoja za upande wa Hamad na wenzake kuwa kiapo pingamizi kilichowasilishwa na Wakili anayeiwakilisha CUF katika kesi hiyo, Twaha Taslima, hakijakidhi viwango vya sheria.
Pia jaji huyo alitupilia mbali pingamizi zote za kisheria za Hamad na wenzake zilizowasilishwa na wakili wao, Augustine Kusalika, dhidi ya kiapo pingamizi cha Taslima.
Baada ya uamuzi huo, Jaji Shangwa aliupa upande wa wadhamini wa CUF kuwasilisha kwa maandishi pingamizi dhidi ya maombi madogo ya Hamad na wenzake ifikapo Machi 15, mwaka huu. Pia Hamad na wenzake wawasilishe majibu ya pingamizi la wadhamini wa CUF ifikapo Machi 23, mwaka huu.
Januari 10, mwaka huu, Hamad na wenzake waliwasilisha maombi mahakamani hapo wakiiomba iwaamuru wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF, akiwamo Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, waitwe mahakamani ili wajieleze ni kwa nini wasitiwe hatiani na kufungwa jela kwa kupuuza amri ya mahakama.
Pia wanaiomba mahakama ibatilishe uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF wa kuwavua uanachama na itamke kuwa wao bado ni wanachama halali wa chama hicho.
Katika kesi ya msingi, Hamad na wenzake wanapinga kuvuliwa uanachama wa CUF na kuiomba mahakama itambue kuwa mkutano uliowafuta uanachama ni batili na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF wafike mahakamani hapo kujieleza kwa nini wasipelekwe jela kutokana na kukaidi amri ya mahakama iliyozuia kufanyika kwa mkutano huo.
CHANZO: NIPASHE