Kesi ya ‘Akinamasamaki wa TRA’ Kuunguruma Januari 13

Mshitakiwa namba moja katika kesi ya kuhujumu uchumi, aliyekuwa naibu wa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Tiagi Masamaki (Kulia) akiwa na wenzake Mahakamani.

Mshitakiwa namba moja katika kesi ya kuhujumu uchumi, aliyekuwa naibu wa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Tiagi Masamaki (Kulia) akiwa na wenzake Mahakamani.


Na Nyakongo Manyama-Maelezo

KESI inayowakabili wafanyakazi wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) inatarajiwa kusikilizwa tena January 13, 2016. Akizungumza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam Wakili wa Serikali Bi. Dianna Lukondo amesema kuwa kwa leo Kesi ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa na kutoa dhamana kwa washtakiwa na hivyo imeshindikana kusikilizwa kutokana na upelelezi kutokamilika.

“Upelelezi haujakamilika hivyo kesi itasikilizwa tena Januari mwakani” alisema Dianna.

Kesi hiyo inawakabili aliyekuwa Naibu Kamishna TRA Tiagi Masamaki, meneja wa kitengo Huduma kwa Wateja Habibu Mponezya, na wengine ni Khamis Omary, Eliaichi Mrema, Burton Kaisi, Harun Mpande na Raymond Louis. Washtakiwa hao wanatuhumiwa kwa kosa la uhujumu uchumi, wakidaiwa kuhusika na upotevu wa makontena 329 katika Bandari ya Dar es Salaam yaliosababisha ukwepaji wa ushuru zaidi ya sh. Bilioni 80.