Kesi dhidi ya Strauss-Kahn yafutwa

Strauss-Kahn

JAJI wa Mahakama mjini New York amefuta kesi ya dhuluma za ngono dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Fedha Duniani, Dominique Strauss-Kahn. Hatua hiyo imejiri wakati waendesha mashtaka walitilia shaka uaminifu wa mwanamke anayemshtaki, ambaye ni mhudumu wa hoteli moja, Nafissatou Diallo , mwenye umri wa miaka 32.

Bw Strauss-Kahn mwenye umri wa miaka 62, alituhumiwa kumshambulia mwanamke huyo, mhamiaji kutoka Afrika, mwezi wa Mei wakati alipokuwa akiingia chumbani kwake kukisafisha. Hukumu hiyo inamaanisha kuwa sasa Strauss-Kahn yuko huru, japo bado anakabiliwa na kesi nyingine dhidi ya Bi Diallo.

”Kushindwa kwetu kuamini mlalamikaji bila ya shaka yoyote kunamaanisha kuwa, hatungeuliza baraza la wazee wa mahakama kutoa uamuzi wao” naibu mwendesha mashtaka alimueleza Jaji.

Kufutiliwa kwa mashtaki ya jinai katika mahakama ya juu mjini New York kutatekelezwa punde baada ya jaji kutoa uamuzi wake wa rufaa iliyokatwa dhidi ya hatua ya leo.

Bw Strauss-Kahn, aliyedhaniwa kuwa mgombea wa urais nchini Ufaransa kabla ya kesi hii kuanza, aliwasili katika mahakama ya Manhattan akiwa kwenye msafara wa magari 6 akiandamana na mkewe Anne Sinclair.

Nje ya mahakama makundi ya waandamanaji walibeba mabango na kukemea uamuzi huo. Katika taarifa aliyoitoa kupitia mawakili wake, Strauss-Kahn amesema” miezi hii miwili na nusu iliyopita imekuwa ni kama jinamizi kwangu na familia yangu”.

”Nataka kuwashukuru mafariki wangu wote nchini Ufaransa na Marekani ambao waliamini kuwa sikuwa na hatia…Ninatoa shukrani zangu kwa mke wangu na familia yangu ambao wamepitia wakati mgumu sana”.

Strauss-Kahn alilazimika kujiuzulu kama mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) baada ya kukamatwa akiwa kwenye ndege ya Shirika la ndege la Ufaransa mwezi Mei.

-BBC