Kero ya maji ‘yawatibua’ nyongo wana-Ludewa

Wananchi wakiwa wamepanga foleni kupata huduma ya maji.

Na Mwandishi Wetu, Ludewa

WANANCHI Ludewa Mjini, mkoani Njombe wamedai hawaoni umuhimu wa kuendelea kuwepo kwa Mamlaka ya Maji Ludewa Mjini (LUDWSSA) kwa sababu inaonekana kushindwa kutoa huduma kwa wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati na mtandao huu, wananchi hao walisema mamlaka hiyo imeshindwa kuwapatia maji ya uhakika, huku serikali ya wilaya hiyo nayo ikisuasua kuchukua hatua kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Ludewa Mjini, Omary Kiowi aliliambia Kwanza Jamii – Njombe kuwa wananchi wake wana haki ya kulalamikia kero hii ambayo sasa inaonekana kudumu kwa muda mrefu.
Benito Mgimba, mkazi wa Mtaa wa Kanisa B, alisema huduma ya maji haijapatikana kwa zaidi ya miaka 10, hivyo kuongeza ugumu wa maisha kwa wakazi hao pamoja na kuwa chanzo cha matatizo mengine kwa jamii.
“Miaka miwili iliyopita tuliambiwa tuchimbe mitaro kwa nguvu zetu wenyewe ili tuletewe maji mtaani, lakini hadi leo hakuna kinachoendelea, tumechimba bure na maji hayaletwi na hakuna taarifa yoyote, ”alilalamika Benito.
Oscar Chaura na Romward Kiowi kwa upande wao walisema watendaji katika idara husika wameshindwa kuwajibika na kwamba hawaoneshi dalili zozote kuhakikisha maji yanapatikana kwa wananchi.
“Katika mtaa wetu wa Kanisa tuliweka bomba la kwanza, lakini watendaji wa mamlaka ya maji wakasema ni dogo, hivyo tukalazimika kuchanga fedha na kununua lingine kubwa, lakini cha ajabu hata baada ya kulitandaz, huu ni mwaka wa 10 bado tunakunywa maji yanayotumiwa na wanyama kama nguruwe, ng’ombe na punda kwenye madimbwi”, alisema Chaura.
Romward Kiowi alilalamika kuwa ni muda mrefu sasa tangu wananchi wa maeneo mengi wachimbe mifereji kwa nia ya kutandaza mabomba, lakini hakuna kinachoendelea, huku madahara ya kutumia maji yasiyokuwa salama yakiongezeka. Magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyokuwa salama ni pamoja na kuugua tumbo na kuhara.
Cathbert Haule, Mkazi wa Mtaa wa Kanisa, Castory Mwachiro wa Mtaa wa Kanisa B, Tiemo Kayanda, Stephano Mahundi, Valentina Mgeni na Lucy Haule kutoka Mtaa a Mkondachi, wameilaumu serikali ya wilaya yao kwa kushndwa kumaliza tatizo la kupatikana kwa maji, huduma ambayo ni muhimu kwa uhai wa maisha ya wananchi.
“Inashangaza na haiingii akilini watendaji wa mamlaka ya maji wanaposema maji hayatoshi wakati yapo baadhi ya maeneo maji yanamwagika ovyo, mimi nadhani hakuna usimamizi wala uwajibikaji kwa watendaji, inawezekana vyanzo havitoshi, lakini ni vyema tukadhibiti maji yaliyopo, jamani watendaji acheni kushinda maofisini,” alilalamika Cathbert .
Akijibu malalamiko hayo, Meneja wa Mamlaka ya Maji Ludewa Mjini (LUDWSSA), Atanasio Munge alikiri kuwapo kwa tatizo la maji katika baadhi ya maeneo ya mji wa Ludewa na kueleza kuwa miundombinu, ikiwamo mambomba yaliyocakaa ndiyo chanzo cha kuwepo kwa kero hiyo kwa muda mrefu.
Pia alieleza kuwa tanki la kuhifadhi maji kabla ya kusambazwa ni dogo na limezidiwa uwezo na ongezeko la idadi ya watu ambao wanaongezeka siku hadi siku katika mji huo wa Ludewa. Munge alisema kutokana na tatizo hilo watu wanaopata maji, tena yakiwa ya mgao ni asilimia 65 ya wakazi wote wa Ludewa, ambao hupata huduma hiyo mara tatu kwa wiki, tofauti na awali wakati idadi ya watu ilikuwa ndogo wakati maji yalikuwa yakipatikana karibu kila siku.
Hata hivyo, alisema mamlaka yake ina mipango kabambe ya muda mfupi na mrefu kukabiliana na kero ya maji mjini kwa kupima na kusanifu chanzo cha maji cha Mapetu na Mwangacha ili kuhakikisha maeneo mengi yanapata maji ya uhakika.
Munge alisema mikakati ya muda mrefu ni pamoja na kuwepo kwa matanki mawili yenye ujazo wa lita 300 ambayo yatajengwa Ludewa (K) na tanki moja lenye ujazo wa lita 1,000 litajengwa Ludewa (M) eneo la Kilimahewa.