Kepteni John Komba Azikwa Wilayani Nyasa, JK Ashiriki
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Machi 3, 2015, ameungana na mamia ya waombolezaji kumzika Mbunge wa Jimbo la Nyasa na msanii mahiri wa muziki nchini, Kepteni John Damiano Komba, kwenye makaburi ya Kanisa Katoliki katika Kijiji cha Lituhi, Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma.
Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Songea, akitokea Dar es Salaam, kiasi cha saa tano na robo asubuhi, Rais Kikwete amekwenda moja kwa moja Lituhi, karibu kiasi cha kilomita 140 kutoka mjini Songea, kwa ajili ya mazishi ya Komba ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Rais Kikwete amejiunga na waombolezaji akiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Semamba Makinda kiasi cha saa tisa mchana kwa ajili ya mazishi ya mmoja wa wasanii ambao walijijengea heshima kubwa kwa nyimbo zake za uhamasishaji.
Wakati wa shughuli za mazishi ambazo kidini zimeongozwa na Askofu John Ndimbo wa Jimbo Katoliki Mbinga, waombolezaji walisomewa salamu za rambirambi ambazo zimetumwa na Rais wa Pili wa Malawi, Mheshimiwa Bakili Muluzi ambaye sasa amestaafu.
Katika salamu hizo, Mheshimiwa Muluzi amesema: “Nilimjua Komba kama rafiki na taarifa za kifo chake cha ghafla zimenistua sana.”
Mwili wa Marehemu Komba uliteremshwa kaburini saa 9:30 mchana huku ukishuhudiwa na mjane wa marehemu Salome Komba na watoto wake 11. Rais Kikwete ameondoka Lituhi mara baada ya mazishi kurejea mjini Songea kumalizia ziara yake ya siku mbili ya kikazi mkoani Ruvuma.