KENYATTA – Isingekuwa Kikwete Historia ya Kenya Ingekuwa Tofauti.

Jakaya-Kikwete

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amemshukuru Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa juhudi na busara zake wakati nchi hiyo ilipoingia kwenye machafuko ya kisiasa mwaka 2007.

Rais Kenyatta amemshukuru Rais Kikwete leo mbele ya wafanya biashara wa Kenya na Tanzania, wakati wakufungua Kikao cha wafanyabiashara pamoja jijini Nairobi leo asubuhi.

“Kama isingekua msaada wako mwaka 2007 na juhudi zako, historia ya Kenya leo ingekua tofauti, asante kwa msaada wako na tunautambua urafiki wetu”. Rais Kenyatta amemuambia Rais Kikwete.

Kenya iliingia kwenye machafuko ya Kisiasa mwaka 2007 kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Nchi hiyo ambapo mapigano na machafuko yalisababisha vifo, uharibifu wa mali na watu kukosa pahali pa kuishi na kusababisha kukimbia makazi yao.

Rais Kikwete aliombwa na Umoja wa Afrika kama mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kusaidia katika juhudi za usuluhishi ambapo hatimaye, pande mbili zilizokua zinazozana ziliunda serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ilileta utulivu na kusitisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Rais Kenyatta pia amemshukuru Rais Kikwete kwa juhudi zake kwenye uwekezaji na kwenye miundombinu ambayo inaimarisha Jumuiya.

Rais Kenyatta pia ametambua na kupongeza juhudi za Rais Kikwete katika kuhamasisha uwekezaji, biashara, miundombinu na uwekezaji kwa ujumla na kueleza kuwa katika kipindi cha miaka 10 ya Rais Kikwete biashara na mauzo ya Kenya Tanzania yameongezeka kwa asilimia 5.5 katika kipindi hicho.

Nae Rais Kikwete amesema anaamini biashara na uwekezaji baina ya Kenya na Tanzania na Afrika Mashariki kwa Ujumla bado unaweza kuongezeka mara tatu zaidi ya sasa.

Rais Kikwete pia ametembelea makao makuu ya jiji la Nairobi na kupokelewa na gavana wa Nairobi Dr. Evans Kidero ambapo amekabidhiwa ufunguo wa jiji la Nairobi na pia kupata heshima ya kuzindua mtaa ulioko maeneo ya Ikulu ambao umepewa jina la Jakaya Kikwete. Mtaa huo ulikua unajulikana kama barabara ya Milimani.

Kabla ya kumkaribisha Rais Kikwete kuzindua barabara hiyo Dr. Kidero amesema Kenya inamshukuru Rais Kikwete kwa dhati na kwamba Ushirikiano wa kibiashara na kijamii ni mzuri sana.

Rais Kikwete anatarajia kuhutubia Bunge la Kenya baadae mchana na kuwaeleza wananchi wote wa Kenya kuwa anatarajia kukabidhi madaraka kwa Rais Mwingine baadae mwaka huu.