Kenya Yazinduwa Treni ya Kisasa Kusafirisha Abiria

Treni ya Kisasa Nchini Kenya

SHIRIKA la Reli nchini Kenya limepiga hatua ya maendeleo kwa usafiri wa treni nchini humo baada ya kuzindua treni mpya ya kisasa ambayo ina mwendo wa kasi itakayo toa huduma kwa wakazi wa viungani vya Jiji la Nairobi. Kwa mujibu wa taarifa zaidi zinasema ni treni ya kwanza ya aina yake kuzinduliwa tangu Kenya kujipatia uhuru mwaka 1963.

Treni hiyo itatoa usafiri kati ya mji mkuu na mtaa wa Syokimau na viunga vyake, viungani mwa Nairobi ambako serikali imejenga kituo cha treni ambacho ni cha kwanza kukamilishwa chini ya mradi wa ukarabati wa mfumo wa reli ambao unafanyika kwa mara ya kwanza kwa miaka 80.

Treni hiyo inanuiwa kupunguza msongamano wa magari mjini Nairobi ambao ni mojawapo ya miji unaokuwa kwa kasi barani Afrika ukiwa na watu zaidi ya milioni tatu. Rais Kibaki aliyefungua rasmi kituo hicho, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuipanda treni hiyo.

Kituo cha treni cha Syokimau ni cha kwanza cha aina yake nchini Kenya, kikiwa na mashine za elektroniki zinazokagua vyeti vya usafiri, pamoja na skirini kubwa ambazo zinatangaza safari za treni. Kila behewa lina uwezo wa kubeba abiria sabini pamoja na miamoja na ishirini watakao simama. Huduma hiyo itakuwa ya kasi na bora zaidi ikilinganishwa na treni za hapo nyuma na pia zitatumia njia tofauti ya reli.

Safari ya kutoka mtaa wa Syokimau inachukua dakika kumi na tano kwa treni hizo huku ikiwa mtu atakwenda kwa gari itamchukua hata masaa mawili. Itamgharimu abiria shilingi miambili kwenda na kutoka mjini.