Kenya yatoa hati ya kukamatwa kwa Bashir

Rais wa Sudan Omary al-Bashir

Mahakama ya Kenya imetoa hati ya kukamatwa kwa rais wa Sudan Omar al-Bashir juu ya madai ya uhalifu wa kivita mjini Darfur.
Uamuzi huo umetolewa baada ya Kenya kumruhusu Bw Bashir kuzuru nchi hiyo mwezi Agosti ikipingana na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC ya kutoa hati ya kukamatwa kwake.
Jaji huyo alisema anatakiwa kukamtwa iwapo “atakanyaga Kenya” tena, shirika la habari la ASP limeripoti.
Kenya ni moja ya nchi zilizotia saini makubaliano ya kuundwa kwa ICC mwaka 2002.
Lakini kama ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika, imekataa kutekeleza makubaliano ya kutolewa hati hiyo ya ICC.
Katika uamuzi wake kutokana na kesi iliyowasilishwa na shirika lisilo la kiserikali, tume ya kimataifa ya wazee wa baraza (ICJ), Jaji Nicolas Ombija alisema kukamatwa kwa Bw Bashir “lazima kuidhinishwe na Mwanasheria Mkuu na waziri wa mambo ya ndani iwapo atakanyaga Kenya”.
Bw Bashir alikuwa rais wa kwanza kushtakiwa na ICC, iliyomtuhumu kwa mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita mjini Darfur.
Bw Bashir anakana mashtaka hayo, akisema yana uchochezi wa kisiasa.
Umoja wa Afrika umejitahidi kuahirisha kutolewa kwa hati hiyo ya kukamatwa, ikiishutumu ICC kufanya utafiti wa madai ya uhalifu wa kivita barani Afrika tu na kusema kumkamata rais wa Sudan kutazuia harakati za kutafuta amani Darfur.
Malawi na Chad ni miongoni mwa nchi nyingine za Afrika ambazo Bw Bashir ametembelea ikipingana na hati yake ya kukamatwa.
Takriban watu milioni 2.7 wamekimbia makazi yao tangu ghasia zilipoanza mjini Darfur mwaka 2003, na umoja wa mataifa umesema takriban watu 300,000 wamefariki dunia -zaidi kutokana na maradhi.
Serikali ya Sudan imesema vurugu hizo zimesababisha vifo vya takriban watu 12,000 na idadi ya waliokufa imetiwa chumvi kwa sababu za kisiasa

-BBC