Kenya yatakiwa kumkamata Henry Banda

Henry Banda

NCHI ya Kenya imepokea ombi kutoka kwa Shirika la Polisi wa Kimataifa Interpol kumkamata mwana wa kiume wa rais wa zamani wa Zambia Rupiah Banda anayeaminika kutorokea nchini humo.

Henry anasemekana kuondoka nchini Afrika Kusini na sasa yuko mafichoni nchini Kenya. Anatafutwa kuhusiana na sakata ya mauzo ya mali ya kampuni ya mawasiliano ya simu ya Zamtel, inayomilikiwa na Serikali.

Haijabainika ni lini, Henry Banda, aliingia nchini Kenya. Hata hivyo Serikali ya Kenya imekanusha kwamba Banda amejificha nchini Kenya.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Kenya Moses Wetangula amesema kuwa mara ya mwisho Henry Banda alitembelea nchini Kenya ilikuwa ni mwezi Novemba mwaka uliopita.

Maafisa wa Kenya wamethibitisha kuwa wamepokea ombi kutoka shirika la Polisi wa Kimataifa (INTERPOL) kumkamata na kumkabidhi bwana Banda kwa maafisa wa polisi nchini Zambia. Anasakwa kuhusiana na kashfa ya uuzaji wa mali ya kampuni ya simu ya nchi hiyo, ZAMTEL.

Kama mmoja wa watu waliokuwa wakihusika na mauzo hayo, Banda anadaiwa kuwa alileta mshauri ambaye alishusha bei ya mali hiyo kwa kiwango kikubwa. Uchunguzi uliofanywa kuhusu mauzo hayo uligundua kulikuwa na udanganyifu mkubwa.

Rais wa sasa Michael Sata ambaye aliahidi kupambana na ufisadi ameapa kusafisha siasa za nchi hiyo na kumaliza rushwa serikalini.
-BBC