Kenya Waadhimisha Miaka 49 ya Uhuru

Rais Mwai Kibaki wa Kenya

SIKU ya Jamhuri ni maadhimisho ya siku Kenya ilipotangazwa kuwa huru baada ya kutawaliwa na wakoloni waingereza waliokuwa wakiwakandamiza waafrika weusi katika taifa hilo la Afrika Mashariki. Leo ni siku ya uhuru wa Kenya, ambapo Wakenya wanaadhimisha miaka 49 ya Siku ya Jamhuri katika sherehe maalum zinazofanyika katika uwanja wa kitaifa wa michezo wa Nyayo.

Rais Mwai Kibaki anawaongoza Wakenya katika kuadhimisha siku hiyo muhimu katika historia ya taifa hilo ikiwa ni tukio lake la mwisho la kitaifa kuliongoza kabla ya kuondoka madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Machi mwaka 2013.

Rais Mwai Kibaki ameitumia siku ya Jamhuri, kama inavyofahamika siku ya uhuru nchini Kenya, kuzungumzia mafanikio yaliyopatikana nchini humo tangu alipoingia madarakani miaka 10 iliyopita, kubwa zaidi ikiwa ni ukuaji wa kiuchumi, maendeleo ya sekta ya miundo mbinu kutokana na miradi iliyoanzishwa katika kipindi hicho cha utawala wake pamoja na kupitishwa katiba mpya mwaka 2010.

Katika hotuba yake isiyopungua dakika 35 pia amewahimiza wananchi wa Kenya kutilia maanani umuhimu wa amani na usalama na kuweka kando tofauti za kikabila katika uchaguzi mkuu ujao huku pia akizungumzia juhudi za serikali katika kupambana na wanamgambo wa kundi la Al-Shabab nchini Somalia ambako jeshi la Kenya linashirikiana na kikosi cha Umoja wa Afrika katika harakati hizo.

Sherehe za mwaka huu za uhuru wa Kenya ni nafasi ya mwisho kwa Rais Mwai Kibaki kulihutubia taifa katika sikukuu ya kitaifa hasa ikizingatiwa sikukuu nyingine ya kitaifa ni Siku ya Madaraka itakayokuwa tarehe 1 Juni mwakani, ambapo atakuwa hayupo tena madarakani.

Kenya ilitumbukia katika ghasia zilizosababishwa na harakati za kuwania madaraka kati ya rais Mwai Kibaki na Raila Odinga baada ya uchaguzi mwaka 2008 kabla ya kufikiwa makubaliano yaliyosimamiwa na jopo maalum la Kimataifa lililoongozwa na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan na hatimae kuundwa serikali ya muungano.

Machafuko baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 yalisababisha kiasi ya watu 1,100 kuuwawa na wengine zaidi ya 65,000 kupoteza makaazi yao.

Sherehe za Jamhuri ni maadhimisho ya kupatikana uhuru wa Kenya tarehe 12 Desemba,1963, kutoka kwa Muingereza baada ya harakati za mapambano ya kundi la Mau Mau zilizoanza katika miaka ya 1950 dhidi ya ukandamizaji uliokuwa ukifanywa na Waingereza. Mau Mau lilikuwa ni kundi la wapiganaji wazalendo lililojumisha zaidi watu wa kabila la Kikuyu ambalo ni kabila kubwa nchini Kenya.

Ni kufuatia mapambano ya Mau Mau dhidi ya viongozi wa kikoloni na walowezi wa Kizungu ambapo katika mwaka 1952 serikali ya kikoloni ilitangaza hali ya hatari na kuwakamata viongozi wengi wa Kenya wa mapambano hayo ya kudai uhuru akiwemo Jomo Kenyatta aliyekuja kuwa rais wa kwanza wa taifa hilo la Afrika Mashariki baada ya uhuru mwaka 1963.

Licha ya migawanyiko ya kikabila, bado Kenya ni taifa kubwa kiuchumi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
-DW