TIMU za Kenya na Uganda zimeingia nusu fainali za mashindano ya Kombe la CECAFA Tusker Chalenji, hivyo sasa zinasubiri kupambana na timu za Tanzania, yaani Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes. Kwa mujibu wa mpangilio baada ya kukamilika michezo miwili ya jana, kwa sasa Kenya itapepetana na Zanzibar Heroes huku Uganda ikiisubiri Kilimanjaro Stars.
Michezo yote miwili ya timu zilizosalia inategemea kuwa na msisimko mkali na kuvuta hisia za wapenzi wa soka kutoka pande mbalimbali. Hata hivyo pamoja na hali zote Uganda ndio timu pekee inayopewa nafasi kubwa kutokana na kucheza nyumbani huku ikiwa na kikosi imara kinachocheza kwa uangalifu mkubwa. Kenya imefanikiwa kuingia hatua hiyo baada ya kuifunga Malawi 1-0, huku Uganda ikiiondoa mashindanoni Ethiopia kwa mabao 2-0.