Na Nicodemus Ikonko, EANA
NCHI mbili tu kati ya tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ndizo pekee, zimetangaza tarehe ya kuwachugua wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) licha ya ukweli kwamba muda wa mwisho wa kufanya zoezi hilo ni Aprili,2012.
Wakati Burundi itachagua wawakilishi wake Aprili 14, Tanzania kwa upande wake itafanya hivyo Aprili 17, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) linaripoti. Nchini nyingine tatu zilizobakia za Kenya, Uganda na Rwanda mpaka sasa hazijapanga tarehe za kufanya uchaguzi wa wawakilishi wao katika bunge hilo.
Kwa mujibu wa barua ya Februari 9, 2012 kutoka kwa Spika wa EALA, Abdirahin Abdi, kwenda kwa Maspika wote wa mabunge ya kitaifa katika nchi wanachama, uchaguzi huo umepangwa kufanyika kabla ya Aprili 14, 2012.
‘’Muda wa uhai wa Bunge la pili la EALA unaisha Juni 4, 2012, na Bunge jipya la tatu, pia litazinduliwa wakati huo,’’ Abdi alisema katika barua ambayo nakala yake imetolewa kwa EANA.
Awamu hii ni zamu ya Uganda kumchagua Spika wa EALA atakayetumikia kwa kipindi cha miaka mitano bila kuomba kuchaguliwa kwa kipindi kingine. Spika wa kwanza alikuwa Abdulrahman Kinana wa Tanzania (2001-2006) na kufuatiwa na Abdi kutoka Kenya.
Waandishi wa habari wa EANA nchini Kenya, Uganda na Rwanda wameripoti kwamba nchi hizo tatu hazijataja tarehe za kufanya uchaguzi wala kutoa orodha ya wagombea wa nafasi hizo.
Dk. Thomas Kashilila, Katibu wa Bunge la Tanzania, aliiambia EANA kwamba uteuzi wa wagombea utafanyika Jumanne ijayo na kisha orodha ya wagombea husika itawasilishwa bungeni Aprili 17, kwa ajili ya uchaguzi.
Chama tawala nchini Tanzania,Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeshachagua wagombea wake 24 watakaoshiriki katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi nane zilizopewa.
Vyama vya upinzani vimetengewa nafasi moja kufikia idadi ya wabunge tisa ambao watakuwa wawakilsihi wa Tanzania katika Bunge la EALA.Nchi nyingine pia zimepewa nafasi tisa kila moja.Miongoni mwa wagombea waliochaguliwa na CCM ni pamoja na Makongoro Nyerere, mtoto wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.
Makongoro hivi sasa ni Mwenyekiti wa CCM katika mkoa alikozaliwa wa Mara, Kaskazini mwa Tanzania, na iwapo atachaguliwa katika bunge la EALA, itarejesha tena ndoto ya baba yake ya kutaka Afrika Mashariki iliyoungana na yenye usitawi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya EANA, Bunge la tatu la EALA linaweza lisiapishwe kwa muda uliopangwa hususan ni kwa sababu ya Uganda ambayo bado inatafuta ushauri wa kisheria juu ya namna ya kuwateua na kuwachagua wawakilishi wao katika bunge hilo.