KENYA imesema kuwa itafuata sera na mfumo wa udhibiti wa madini kama unaotumiwa na Tanzania kwa sababu mageuzi yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania katika sekta ya madini ni dhahiri kuwa yameanza kuzaa matunda.
Aidha, Kenya imewashauri Watanzania kuwa wakati ni kweli kuwa ni vyema kupata Katiba Mpya lakini Katiba peke yake haiwezi kuleta maendeleo ya wananchi na kuwa maendeleo yataletwa na juhudi zenyewe za wananchi.
Hayo yamesemwa Agosti 23, 2013 na Balozi wa Kenya katika Tanzania, Mutinda Mutiso wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Ikulu, Dar Es Salaam.
Mutiso alikuwa anamwaga Rais Kikwete baada ya kumaliza muda wake wa kuwa Balozi wa Kenya katika Tanzania kwa kipindi cha miaka minne unusu.
Katika mazungumzo hayo, Balozi amemwambia Rais Kikwete kuwa wataalam wa madini wa Kenya tayari wamekuja Tanzania kujifunza sera za madini na udhibiti wake kwa sababu dunia nzima inajua kuwa mageuzi ambayo Tanzania ilifanya katika sekta ya madini zimezaa matunda.
“Sisi katika Kenya hatukutaka kwenda mbali katika nchi nyingine wakati ujuzi wa shughuli za kufanya mageuzi katika sekta ya madini uko katika nchi jirani ya Tanzania. Mheshimiwa Rais mageuzi ambayo mliyafanya katika sekta ya madini ni dhahiri sasa kuwa yanazaa matunda,” amesema Mheshimiwa Balozi Mutiso na kuongeza:
“Kwa sababu hiyo sisi katika Kenya tunaiga kila ujuzi na uzoefu wa Tanzania katika maandalizi ya kufanya mageuzi katika sekta yetu ya madini.”
Kuhusu suala la jitihada za kutafuta Katiba Mpya, Balozi huyo ameipongeza Tanzania na Watanzania kwa jitihada zinazofanywa sasa kutafuta Katiba mpya. “Tunawatakia kila la heri kwa sababu sisi tulichukua muda mrefu sana kupata Katiba Mpya kama unavyojua Mheshimiwa Rais.”
Ameongeza Mheshimiwa Mutiso: “Kubwa ambalo sisi katika Kenya tumejifunza katika michakato ya namna hiyo ni kwamba Katiba siyo ugali ambao wananchi wanaweza kula moja kwa moja. Katiba ni nyaraka muhimu ya kuelezea mfumo wa utawala na uendeshaji wa nchi.”
Amesisitiza: “Lakini Katiba pekee haileti maendeleo. Maendeleo ni matunda ya juhudi na jitihada za wananchi siyo matunda ya kuwepo kwa Katiba Mpya.”
Mbali na kuagana na Balozi Mutinda Mutiso, Rais Kikwete pia ameagana na Balozi wa Italia katika Tanzania, Mheshimiwa Pierluigi Velardi ambaye anaondoka nchini baada ya kuiwakilisha nchi yake miaka mitatu.
Katika mazungumzo na Balozi Velardi, Rais Kikwete ameishukuru Italia kwa kuunga mkono jitihada za maendeleo za Tanzania kwa kugharimia miradi mbali mbali ikiwemo ujenzi wa Barabara ya Dar-Bagamoyo na kuunganishwa kwa umeme kutoka Tanzania kwenda Bukoba. Wakati huo huo, Rais Kikwete amewasili Dodoma kwa ziara ya siku tatu ya kikazi katika mkoa huo.