Kemikali Zikitumika Ipasavyo Zitapunguza Athari kwa Watu na Mazingira.

Meneja wa Kanda ya Mashariki,Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Bw. Daniel Ndiyo

Meneja wa Kanda ya Mashariki,Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Bw. Daniel Ndiyo


Na Jovina Bujulu- MAELEZO
Kukosekana kwa uelewa juu ya hatari na madhara yanayoweza kusababishwa na kemikali kumetajwa kuwa ni chanzo kikubwa cha ajali mbali mbali hapa nchini.

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Ndugu Daniel Ndiyo alipokuwa akizungumzia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na uthibiti wa kemikali.

“Chanzo kikubwa cha ajali na matukio mengi ya kemikali yanayotokea yanatokana na kukosekana kwa uelewa juu ya hatari na madhara yanayoweza kusababishwa na kemikali hizo”

“Ajali hizo zinaweza kuzuilika endapo wananchi watapatiwa elimu na uelewa wa matumizi au usimamizi sahihi na salama wa kemikali hizo” alisema ndugu Ndiyo.

Akizungumzia ajali hizo, kwa kipindi cha mwaka 2014, ndugu Ndiyo alitoa mfano wa matukio na ajali zipatazo 11 zilizotolewa taarifa ambazo zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 14 pamoja na uharibifu mkubwa wa mali ikiwemo kuungua moto kwa magari na tani zaidi ya 250 za kemikali.

Akizungumzia hatua za utekelezaji, usimamizi na udhibiti wa wa kemikali ndugu Ndiyo alisema kuwa sheria na kanuni ya kemikali ya mwaka 2015, inaagiza kuwa kila anayehusika na kemikali kwa kuingiza kutoka nje, kusafirisha, kuuza, kusambaza, kutumia au kwa namna yoyote ile ni lazima awe amesajiliwa na Mkemia Mkuu wa Serikali nchini.

Aidha Ndugu Ndiyo alisema kuwa baada ya kupitishwa kwa sheria na kanuni za kemikali kumekuwa na mafanikio mbali mbali ikiwa ni pamoja na udhibiti wa kemikali zinazoingizwa nchini tangu usafirishaji, utumiaji na hata uteketezaji wake.

“Hatua hii imesaidia kutambua mapema kemikali zinazoingia nchini, mahali zinapokwenda na matumizi yake, hatua ambayo imesaidia kuzuia kemikali hatarishi ambazo zinaweza kuleta madhara kwa watu na mazingira kuingia na kutumika nchini” aliongeza ndugu Ndiyo.

Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa kemikali za Viwandani na Majumbani Sura 182 ilitungwa ili kuhakikisha kuwa kemikali zinatumika katika hali iliyo salama bila kuleta athari kwa watu na mazingira.