Kazi ya Gesi Yetu ni Kufuta Umasikini – JK

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa jukumu kubwa la gesi asilia nyingi iliyogunduliwa na inayoendelea kugunduliwa maeneo mbali mbali nchini ni kuwatoa Watanzania katika umasikini. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni lazima wananchi waweze kuona na kuthibitisha manufaa ya gesi hiyo kwa maendeleo yao katika kipindi kifupi.

Pia Rais Kikwete amesema kuwa uchochezi wa baadhi ya wanasiasa kuhusiana na gesi asilia iliyogunduliwa nchini ni changamoto ambayo, hata hivyo, Serikali yake iko tayari kupambana nayo. Rais Kikwete alitoa msimamo huo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kundi la Makampuni ya British Gas (BG) Bwana Chris Finlayson, moja ya makampuni ambayo yamegundua gesi na yameanza kuwekeza katika uchimbaji wa raslimali hiyo muhimu.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Rais Kikwete alimwambia Bwana Finlayson na ujumbe wake kuwa gesi asilia hiyo inayoendelea kugunduliwa nchini ni raslimali muhimu na lazima itumike katika “kuwatoa watu wetu katika umasikini na lazima ibadilishe maisha yao.”
Aliongeza Rais Kikwete: “Hivyo, maandalizi ya uchimbaji wake yasichukue muda mrefu …..miaka 10 hivi….. huu ni muda mrefu sana kwa sababu wananchi wetu wanahitaji kuona manufaa ya gesi asilia hiyo katika kipindi kifupi iwezekanavyo”.

Aliongeza Rais Kikwete: “Ni dhahiri kuwa nyie wabia wetu mtanufaika na gesi asilia hiyo kutokana na uwekezaji wenu lakini kimsingi tunataka gesi hii iwanufaishe watu wetu, iwatoe katika umasikini. Kama gesi hiyo inaweza kutuingizia pato la dola za Marekani bilioni moja kwa mwaka, ni dhahiri tunaweza kuibadilisha nchi hii ikawa mbingu.”

Kuhusu wanasiasa wachochezi ambao wamekuwa wanawachochea wananchi wa Mtwara kudai kuwa gesi isitoke katika Mkoa huo na kuwa itumike kwa manufaa yao pekee, Rais Kikwete alisema: “Uchochezi wa wanasiasa ni changamoto. Hakuna shaka. Lakini hii ni changamoto ambayo Serikali itapambana nayo na ina uwezo wa kutosha wa kumaliza changamoto hiyo.”

Naye Bwana Finlayson alimweleza Rais maendeleo ya maandalizi ya uchimbaji wa gesi asilia hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi za masomo kwa vijana wa kitanzania kusomea utaalamu mbali mbali wa gesi hiyo asilia.