Kauli ya UVCCM yaleta ‘utata’ CCM Arusha

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi, Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda

Na Janeth Mushi, Arusha

KAULI iliyotolewa na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) imeibua mjadala baada ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi, Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, kuwataka UVCCM kutambua kuwa matatizo ya umoja huo hayawezi kupatiwa ufumbuzi nje ya chama hicho.

Katibu huyo ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM) mkoani Tanga
ameongeza kwamba matatizo yoyote ya CCM yanapasa kushughulikiwa ndani ya chama kupitia vikao mbalimbali akiwemo yeye binafsi hivyo kukabidhi jukumu hilo kwa Mbunge Lema ni sawa na kwamba amekubali kushindwa kutatua
matatizo na changamoto zinazowakabili vijana.

Mwenyekiti wa UVCCM taifa Beno Malisa juzi akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Hospitali ya Mtakatifu Thomas Arusha alisema mshikamano na umoja ndani ya Jumuiya hiyo hauwezi kuendelea kama hautafanyika ushirikiano na mbunge wa Jimbo la Arusha mjini, Godbles Lema (CHADEMA).

Akifafanua Chatanda alimtaka Malisa kuheshimu mamlaka anuai zilizopo ikiwemo uongozi wa Chama na Jumuiya zake na kwamba suala la mgogoro wa Arusha awaachie viongozi wa mkoa huu na kama akihitaji kutoa msaada alipaswa kufika mkoani hapa na kutoa taarifa kwa uongozi ili kushirikishwa badala ya yeye kufanya kazi hiyo bila taarifa.

Katibu huyo alihoji iweje agizo la Malisa litekelezwe wakati yeye
binafsi amekuja katika wilaya na mkoa wa watu bila taarifa kwa uongozi
ambapo alimsihi Malisa kubadilika kwanza ndipo atoe maagizo kama hayo.

Malisa alisema maneno hayo katika mkutano wa majumuisho ya ziara yake
ya uzinduzi wa mashina ya wakereketwa wa UVCCM jijini Arusha juzi
ambapo aliambatana na viongozi wenzake mbalimbali ambapo walifungua
mashina 22 katika kata mbalimbali katika Manispaa ya Arusha.

Katika ziara hiyo Malisa aliambatana na Naibu Katibu Mkuu UVCCM Zanzibar Jamal Ally, Mbunge wa Viti Maalumu Vijana mkoa wa Arusha Catherine Magige, mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Kilimanjaro Godlivin Moshi, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Morogoro, Jonas Nkya, mjumbe wa baraza kuu UVCCM John Nchimbi, mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha James Ole Millya, katibu wa UVCCM Mkoa wa Arusha Abdalah Mpokwa na makatibu wa jumuiya hiyo wilaya za Arusha.