KAULI YA SERIKALI BUNGENI KUHUSU TAARIFA YA AWALI YA TUME YA TAIFA YA KUCHUNGUZA MATOKEO YA MTIHANI WA TAIFA WA KIDATO CHA NNE MWAKA 2012
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 49(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2007, naomba kuwasilisha Taarifa ya Awali ya Tume ya Taifa ya kuchunguza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012.
2. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa Matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2012 yalionesha kuwa kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni. Matokeo yaliyotangazwa mwezi Februari, 2012 yalionesha kwamba kati ya Wanafunzi 367,756 waliofanya mtihani huo, Watahiniwa 126,847 ndio waliofaulu. Katika idadi hii, Wanafunzi waliofaulu katika Daraja la Kwanza hadi la Tatu ni 23,520, sawa na Asilimia 6.4 na Daraja la Nne ni 103,327, sawa na Asilimia 28.1. Watahiniwa 240,909, sawa na Asilimia 65.5 ya Wanafunzi wote waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 walipata Daraja la Sifuri.
3. Mheshimiwa Spika, kushuka kwa kiwango cha ufaulu kulihusu shule za aina zote, yaani Sekondari za Serikali ikijumuisha zilizojengwa kwa nguvu za Wananchi, Shule Binafsi na Seminari. Takwimu zinaonyesha kwamba ukilinganisha matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2011 na mwaka 2012, Shule za Wananchi matokeo yao yameshuka kwa Asilimia 1.82; Shule za Umma za zamani (Kongwe) yameshukwa kwa Asilimia 6.43; Shule Binafsi yameshuka kwa Asilimia 6.39; na kwa Shule za Seminari yameshuka kwa Asilimia 7.29. Hali hii inaonyesha kwamba, matokeo katika Shule za Wananchi yameshuka kwa kiwango kidogo ikilinganishwa na yale ya Shule za Umma za zamani (Kongwe), Shule Binafsi na Shule za Seminari ambazo zilitegemewa kufanya vizuri zaidi ya zile za Wananchi ambazo matokeo yao yameshuka zaidi kwa kati ya Asilimia 6.4 na 7.3.
4. Mheshimiwa Spika, kutokana na matokeo hayo yasiyoridhisha na ambayo yapo nje kabisa ya mwenendo wa ufaulu kwa miaka ya karibuni, Serikali iliamua kuunda Tume ya Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha Ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012 kwa madhumuni ya kupata ufumbuzi wa kudumu.
HADIDU ZA REJEA
5. Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchunguzi ilipewa Hadidu za Rejea zikiwemo zifuatazo:
i. Kubainisha sababu za matokeo mabaya ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012;
ii. Kubaini sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2011 hadi 2012;
iii. Kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua kukabiliana na tatizo la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu mara moja, kipindi cha muda mfupi, kati na kipindi cha muda mrefu;
iv. Kutathmini nafasi ya Halmashauri katika kusimamia Elimu ya Sekondari katika Halmashauri zake;
v. Kuanisha sababu nyingine zinazoweza kuwa zimechangia hali hii ya matokeo.
6. Mheshimiwa Spika, katika kutafakari Hadidu za Rejea hizo, Tume imejikita katika kujibu Maswali Makuu matatu.
i) Kwa nini matokeo ya Kidato cha Nne kuanzia mwaka 2008 yamekuwa na mserereko wa kushuka kuliko miaka iliyotangulia?
ii) Kwa nini Wanafunzi wa Kidato cha Nne wa mwaka 2012 matokeo yao yalikuwa mabaya kuliko ya wenzao wa mwaka 2011 pamoja na kwamba ufaulu ulishuka tangu mwaka 2008? na
iii) Nini kifanyike.
WAJUMBE WA TUME YA UCHUNGUZI
5. Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchunguzi iliongozwa na Prof. Sifuni Mchome kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania na ndiye alikuwa Mwenyekiti. Wajumbe wengine waliteuliwa kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu, Baraza la Wawakilishi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Madhehebu ya Dini, Chama cha Walimu, Muungano wa wenye Shule Binafsi na Muungano wa Walimu wa Sekondari. Orodha ya Wajumbe wa Tume hiyo ni kama ifuatavyo:
NA. JINA TAASISI ANAYOTOKA NAFASI
1. Prof. Sifuni Ernest Mchome Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania Mwenyekiti wa Tume
2. Mhe. Bernadeta K. Mushashu (Mb.) Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Makamu Mwenyekiti
3. Mhe. Abdul J. Marombwa (Mb.) Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mjumbe
4. Mhe. Suleiman H. Hamisi (MBLW) Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mjumbe
5. Mwalimu Honoratha Chitanda Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mjumbe
6. Ndugu Rakesh Rajani
TWAWEZA Mjumbe
7. Mwalimu Daina W. Matemu Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania Mjumbe
8. Mwalimu Kizito Innocent Lawa Taasisi ya Elimu Tanzania Mjumbe
9. Mwalimu Mabruki J. Makame
Baraza la Elimu Zanzibar Mjumbe
10. Prof. Mwajabu K. Possi
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mjumbe
11. Mwalimu Nurdin Mohamed Chuo cha Ualimu cha Al-Harmain Mjumbe
12. Ndugu Peter Maduki Baraza la Kikristo la Huduma za Jamii Mjumbe
13. Ndugu Mahmoud A. K. Mringo Chama wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali Mjumbe
14. Ndugu Abdallah H. Mohamed Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar Mjumbe
TAARIFA YA TUME YA UCHUNGUZI
6. Mheshimiwa Spika, tarehe 28 Aprili, 2013 Tume ya Uchunguzi wa Matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2012 ilikamilisha kazi yake katika Awamu ya Kwanza na kutoa Taarifa ya Awali. Uchambuzi wa Taarifa hiyo ya awali unaonesha kuwa kutokana na Uchunguzi uliofanyika, kwa muhtasari Tume imebaini mambo muhimu yafuatayo:
6.1 Matokeo ya Kidato cha Nne kuanzia mwaka 2008 yamekuwa na mserereko wa kushuka kuliko miaka iliyotangulia kwa sababu mbalimbali ikiwemo changamoto zinazotokana na mafanikio yaliyopo sasa ya kuongezeka sana kwa Idadi ya Shule za Msingi na za Sekondari, hususan kati ya mwaka 2001 na sasa (2013); na hivyo kuwa na idadi kubwa ya Wanafunzi waliopo Shuleni.
Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 1961 hadi 2001 Idadi ya Wanafunzi wa Shule za Msingi imeongezeka kutoka Wanafunzi 486,470 (1961) hadi 4,875,764 mwaka 2001, sawa na ongezeko la Wanafunzi 4,389,294 katika kipindi hicho cha takriban miaka 40. Hata hivyo, kati ya mwaka 2001 hadi 2012 Wanafunzi wameongezeka kutoka 4,875,764 mwaka 2001 hadi 8,247,472 mwaka 2012, sawa na ongezeko la Wanafunzi 3,371,708 katika kipindi cha takriban miaka 11 na hivyo kufanya jumla ya Wanafunzi wote wa Shule za Msingi kuwa 8,247,472 mwaka 2012.
Kuhusu Shule za Sekondari Idadi ya Wanafunzi imeongezeka kutoka 11,832 mwaka 1961 hadi 289,699 mwaka 2001 ambayo ni sawa na ongezeko la Wanafunzi 274,867 katika kipindi hicho cha miaka 40. Lakini kati ya mwaka 2001 hadi 2012 Idadi ya Wanafunzi imeongezeka kutoka 289,699 (mwaka 2001) hadi 1,884,270 mwaka 2012, sawa na ongezeko la Wanafunzi 1,594,571 katika kipindi cha miaka 11 tu.
Juhudi hizi zimetokana na Mipango mbalimbali iliyoandaliwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu wa mwaka 1999. Mipango hii ni pamoja na:
1. Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) wa mwaka 2002 ambapo:
a) MMEM I ambayo ililenga katika kufungua Shule zaidi ili Wanafunzi wengi wa rika lengwa waweze kujiunga na Elimu ya Msingi;
b) MMEM II ambayo ililenga katika kuboresha ubora wa elimu itolewayo katika Shule za Elimu ya Msingi; na
c) MMEM III ambayo ililenga katika kuendelea kuimarisha ubora wa Elimu ya Msingi baada ya mafanikio ya MMEM I na MMEM II.
2. Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) wa mwaka 2004 ambapo:
a) MMES I ambayo ililenga katika kufungua Shule zaidi za Sekondari katika ngazi ya Kata ili Wanafunzi wengi zaidi wanaomaliza Elimu ya Msingi waweze kujiunga na Elimu ya Sekondari Kidato cha Kwanza; na
b) MMES II ambayo ililenga katika kuendelea kuimarisha ubora wa Elimu ya Sekondari kadri Idadi ya Wanafunzi wa Elimu ya Sekondari wanavyoendelea kuongezeka.
Changamoto zinazoambatana na mafanikio haya ni pamoja na mazingira yasiyoridhisha ya kufundishia na kujifunzia, ikiwemo upungufu wa miundombinu muhimu ya shule kama vile Madarasa, Maabara, Madawati, Maktaba, Nyumba za Walimu, Hosteli na majengo mengine muhimu ya Shule. Vilevile, kuna tatizo la uhaba wa Walimu, Vitabu, zana za kufundishia na matatizo ya Ukaguzi wa Shule. Vilevile, Tume imebaini kuwa Mfumo wa Elimu ya Msingi na Sekondari unakabiliwa na changamoto nyingine mbalimbali ambazo Taifa inapitia kwa sasa ikiwemo masuala ya Kisera, Kisheria, Kimfumo, Kimuundo pamoja na changamoto za uhaba wa Rasilimali Fedha na Rasilimali Watu. Tume inaendelea kufanyia kazi maeneo haya kwa kushirikiana na Wataalamu na Wadau wengine;
6.2 Kuhusu matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2012, Tume imebaini kwamba, pamoja na Wanafunzi hawa kuwa katika mazingira yanayofanana na ya wenzao wa miaka iliyopita na kwamba ufanisi katika shule kwa ujumla umekuwa unashuka kwa sababu mbalimbali, ufaulu wao umeshuka zaidi kwa sababu ya mabadiliko ya mchakato wa kuandaa na kutoa matokeo ya mtihani kwa mwaka 2012. Mfumo uliotumika mwaka 2012 katika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na ule uliotumika mwaka 2011 na miaka iliyotangulia. Uchunguzi unaonesha kuwa mwaka 2011, Baraza la Taifa la Mitihani lilikuwa linachakata Alama za mwisho kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa unabadilika kutegemea hali ya ufaulu wa Mwanafunzi ambao ni “National Mean Difference” (NMD). Utaratibu huu ulitokana na tofauti ya Wastani wa Kitaifa wa Alama za Maendeleo kutoka Alama za Maendeleo Endelevu (Continued Assessment – CA) za Watahiniwa wote na Wastani wa Kitaifa wa ufaulu wa Mitihani ya mwisho kwa somo husika. Kila Mtahiniwa aliongezewa “National Mean Difference” iliyokokotolewa katika Alama za Mtihani wa mwisho ili kupata Alama itakayotumika kupata Daraja la ufaulu. Kimsingi, kila somo lilikuwa na NMD yake kulingana na Continued Assessment (CA) zilivyo kwa mwaka husika.
Lakini mwaka 2012 Baraza lilitumia Mfumo Mpya ambao ulikuwa haubadiliki kutegemea hali ya ufaulu wa Mwanafunzi, yaani kuwa na Viwango Maalum vya Kutunuku (Fixed Grade Ranges). Tume imebaini kwamba, pamoja na kwamba Mfumo huo uliandaliwa kwa nia nzuri, Utaratibu huo mpya haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika.
MAPENDEKEZO YA AWALI YA TUME
7. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia masuala mbalimbali yaliyojitokeza wakati wa uchunguzi, Tume katika Taarifa yake ya awali imetoa mapendekezo mbalimbali yakiwemo yale yanayohitaji kutekelezwa kwa haraka. Kutokana na kuwepo kwa mapendekezo hayo ambayo inabidi yafanyike kwa haraka, tarehe 29 Aprili, 2013 Baraza la Mawaziri lilipokea Taarifa ya Awali ya Tume na kuijadili ambapo liliridhia mapendekezo hayo yaanze kutekelezwa mara moja. Maamuzi hayo ya Baraza la Mawaziri yanalenga kutenda haki kwa Walimu na Wanafunzi ambao juhudi zao za kufundisha na kujifunza zimepimwa kwa kutumia Mfumo mpya ambao hawakupata fursa ya kushirikishwa na kuandaliwa. Mapendekezo hayo ni yafuatayo:
i. Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 yafutwe na yaandaliwe upya kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011;
ii. Standardisation ifanyike ili matokeo ya Wanafunzi yalingane na juhudi walizoziweka katika kusoma kwa mazingira na hali halisi ya Tanzania na uamuzi wa Taifa kuongeza idadi ya Shule na Wanafunzi wakati uwekezaji katika ubora unaendelea;
iii. Baraza la Taifa la Mitihani limeelekezwa kuzingatia kuwa pamoja na kwamba Sheria ya kuanzishwa kwake inawaruhusu kufanya marekebisho ya mchakato wa mitihani, lakini marekebisho yoyote ya kubadilisha Utaratibu wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya Mitihani, lazima yahusishe Wadau wote wanaohusika na Mitaala, Ufundishaji na Mitihani.
Wakati Tume inaendelea kukamilisha kazi yake, uamuzi wa Baraza la Taifa la Mitihani wa kutumia utaratibu mpya wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya Mitihani uliotumika mwaka 2012 usitishwe na badala yake Baraza la Mitihani litumie Utaratibu wa mwaka 2011 kwa Kidato cha Nne na cha Sita kwa Mitihani yote ukiwemo utaratibu wa Standardization na kutoa Matokeo mapya kwa kuzingatia maelekezo haya.
Aidha, mchakato wa Mfumo wa Tuzo wa Taifa (National Qualifications Framework) na Mfumo wa kutahiniwa/kutathmini maendeleo ya Mwanafunzi katika masomo yake (National Assessment Framework) ukamilishwe haraka iwezekanavyo.
UTEKELEZAJI WA MAPENDEKEZO YA TUME
8. Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa mapendekezo hayo, Baraza la Mawaziri limeamua kwamba utekelezaji wa mapendekezo hayo uanze mara moja.
9. Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchunguzi itaendelea kukamilisha Taarifa yake vizuri kwa kuhusisha Wadau mbalimbali ili kupata maoni zaidi na ushauri wao juu ya mambo mbalimbali yaliyobainika wakati wa uchunguzi kabla ya kuikamilisha na kuitoa kwa matumizi ya Umma na Vyombo mbalimbali.
HITIMISHO
10. Mheshimiwa Spika, Serikali inaipongeza sana Tume kwa kutoa mapendekezo ya awali ambayo Serikali imeyaridhia. Aidha, Serikali inawashukuru Wananchi wote na Wadau mbalimbali wa Sekta ya Elimu wanaoendelea kutoa maoni na ushauri wao kwa Tume.
11. Mheshimiwa Spika, Serikali inawahakikishia Wananchi kuwa itaendelea kuboresha Elimu Nchini ili kuwezesha Watoto wetu wapate mafanikio katika maisha na maendeleo yao, kwani Wahenga wanasema “Elimu ni Ufunguo wa Maisha”.
12. Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.