WAKATI tayari Mbwana Samatta akiwa amepatiwa viza na Ubalozi wa Ubelgiji kwenda kusaini klabu ya KRC Genk, mshambuliaji Mbwana Ally Samatta anaweza akabaki TP Mazembe ya DRC kumalizia Mkataba wake hadi Aprili.
Hiyo inatokana na Rais wa Mazembe, Moise Katumbi kugoma kumuuza Mwanasoka huyo Bora Anayecheza Afrika katika klabu hiyo Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Katumbi anataka Samatta aende Nantes FC ya Ligi Kuu ya Ufaransa, ambayo amekwishafikia makubaliano nayo, na wiki iliyopita Nantes FC ilituma mwakilishi wake Dar es Salaam, ambaye alifanya mazungumzo na Meneja wa Samatta, Jamal Kisongo mbele ya Ofisa mmoja wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Katika mazungumzo, Kisongo alifikia makubaliano ya maslahi binafsi na Samatta ikiwemo dau la kusaini, mshahara, masharti na marupurupu mengine.
Kisongo alitaka kiwepo kipengele cha mchezaji kutorejeshwa Afrika iwapo hatapata nafasi ya kucheza Nantes, bali auzwe klabu nyingine ya Ulaya na ikakubaliwa.
Nantes ilionyesha nia ya dhati kabisa ya kumchukua Samatta na Kisongo aliinuka kwenye meza ya mazungumzo akiwa amekubali na kusema anakwenda kuzungumza na mchezaji.
Hata hivyo, inaonekana Samatta mwenyewe ndiye anayetaka kwenda Ubelgiji na si Ufaransa, kwani kitendo cha Kisongo kutorejesha majibu kwa Nantes kinaashiria ameshindwa kumshawishi mchezaji wake akubali ofa hiyo.