KATIBU wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Thomas Kashililah amesema wabunge wengi kutofahamu vema kanuni za uendeshaji wa Bunge, ndiyo chanzo cha mivutano na vijembe kutawala vikao vya Bunge la 10.
Kashililah alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa hali hiyo pia inachangiwa na uwepo wa wabunge wengi vijana, umelifanya Bunge kuonekana kama la wanafunzi. Tangu kumalizika kwa vikao vya Bunge la 10, wadau na wananchi wamekuwa wakikosoa mambo yaliyokuwa yakifanyika wakati wa Bunge hilo.
Katika Bunge hilo, baadhi ya wabunge walionekana kwenda kinyume cha kanuni na kuzusha majibizano yaliyoambatana na vijembe bila kuheshimu kiti. Wabunge hao walikwenda mbali zaidi pale baadhi walipotaka milango ya ukumbi ifungwe ili wachapane makonde kufuatia kushindwa kuafikiana katika baadhi ya mambo.
Dk. Kashililah alisema Bunge la 10 mkutano wa tatu linapaswa kuwa na wabunge 357 na kwamba, waliopo kwa sasa ni 350 huku asilimia 70 wakiwa ni wageni na vijana, ambao hawana uzoefu na mijadala.
Hata hivyo, alisema kuwa yaliyotokea katika Bunge hilo hayakusababishwa na udhaifu wa Spika Anne Makinda kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Pia, alisema kuwa Spika Anne alitumia busara na uzoefu wa hali ya juu katika kuweka sawa mambo yaliyokuwa yakijitokeza. Spika ana mamlaka ya kumsimamisha mbunge asihudhurie vikao 10, iwapo atakiuka kanuni, lakini hakufanya hivyo kwa kuwa wabunge wengi bado wanajifunza,” alisema.
Alisema kanuni imeweka wazi kuwa Spika wa Bunge anaposimama, mbunge anayezungumza anapaswa kuacha kuongea na kukaa, lakini hilo lilikuwa likikiukwa. Alisema kuna wakati Spika Anne alikuwa akisimama kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali, lakini wabunge nao wanasimama kwa kutofahamu taratibu.
“Hivi katika bunge la namna hiyo, utatoa adhabu kwa watu ambao unajua wapo darasa la kwanza, na mwingine anaibuka na kusema funga mlango tupigane, hawa wanapswa kufundishwa,” alisema Kashillilah.
Akizungumzia Muswada wa Marejeo ya Katiba, alisema vurugu zilizojitokeza katika vituo vya kukusanyia maoni ya wananchi, Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar zilisababishwa na upotoshwaji wa muswada huo.
“Naomba ieleweke kuwa Rais Jakaya Kikwete alitoa heshima kwa wananchi kutoa maoni yao katika mchakato wa kuunda kamisheni ya kukusanya maoni, lakini baadhi ya wachangiaji walifikiri ndio muswada wa katiba mpya,” alisema.
Alisema katika mkutano huo, miswada sita ilipelekwa bungeni, lakini wa katiba na ule wa marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma haikupitishwa kutokana na muda mdogo wa kuijadili.