Katibu Tawala Ruvuma azindua mashine ya kukamua alizeti kwa Wana-vijiji

Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Dk. Aselm Tarimo akiambatana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Ruvuma akielekea kuzindua mashine ya alizeti Mtyangimbole.

Na Dunstan Mhilu, Ruvuma

KATIBU Tawala Mkoa wa Ruvuma, Dk. Aselm Tarimo juzi amezindua mashine za kukamua mafuta ya alizeti katika Kijiji cha Mtyangimbole Wilaya ya Songea Vijijini. Katika uzinduzi huo aliwataka wananchi wa kijiji hicho na vijiji vya jirani kuhakikisha wanaitumia vizuri mashine hiyo ili iweze kuwanufaisha kihuduma.

“Mashine imeletwa kazi ni kwenu, …leteni alizeti yenu ikamuliwe mpate mafuta safi ya kutumia na kuuza haijalishi kuwa wewe ni mwana kikundi au la mashine ni mali ya kikundi, lakina ina hudumia wananchi wote. Na ni vema mkahakikisha kipindi hiki ambacho mvua zimeanza kunyesha mnalima hekari nyingi iwezekanavyo,” alisema Tarimo.

Aidha amewaeleza kuwa chakula kwa sasa ni mali nzuri kwani gunia la mahindi lililokuwa likiuzwa sh. 3000 kwa sasa linauzwa sh. 25,000 hadi 30,000; kadhalika alizeti zamani iliyokuwa ikichukuliwa zao la kawaida hivi sasa inafanya vizuri sokoni (inalipa) mbegu ya alizeti kilo moja huuzwa sh. 5000 na huku lita moja ya mafuta yake ikiwa ni sh. 3500. “Hii inaonesha ni kwa jinsi gani alizeti inalipa,” alisema mkuu huyo.

Naye Ofisa Ugani wa Halmashauri ya Songea Vijijini, Leonard Makumi amewataka wananchi hao kulima alizeti kwa wingi na kudai endapo itatokea tatizo lolote kuhusu magonjwa au ushauri wowote ofisi yake ipo wazi na maofisa ugani kuanzia ngazi ya kata na kijiji kuwasaidia.

“Watumieni maofisa ugani mlio nao, maofisa wa MUVI hata kwakuwatembelea ofisini kwao japo kuwa wanawatembelea mara kwa mara wao kwani wapo katika kipindi cha uhamasishaji kwa vijiji vya Mpandangindo na Mtyangimbole, kwani tulishafanya zoezi hili vijiji vingine ambavyo vipo ndani ya mradi,” amesema.

Muunganisho wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) hivi karibuni umefunga mashine nane, ambapo tano zikiwa zimenunuliwa na MUVI mbili zimenunuliwa na DADPS, wakati moja ni mkopo kutoka SIDO mashine zilizo nunuliwa na Muvi ni Kilosa Mbabay Kilosa, Mkako hizi zikiwa ni wilaya ya Mbinga, Namtumbo ni kijiji cha Hanga, kwa Songea Vijijini ni Lundusi na Matimira.

Zilizo nunuliwa na DADPS ni za mpandangindo na mtyangimbole kwa Songea vijijin wakati Namtumbo katika kijiji cha Utwango ni mali ya wana kikundi kutoka SIDO MUVI imechukuwa jukumu la kufunga mashine zote na kumlipa fundi kama sehemu ya ushirikiano na DADPS ikiwa ni kuunga mkono juhudi za wana vikundi hao.