Na Lorietha Laurence – Maelezo
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka wamiliki wa radio kuhakikisha kuwa wanafuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji pamoja na kuandaa vipindi vyenye maudhui yanayoelimisha na kujenga jamii.
Aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya radio yaliyoratibiwa na shirika la UNESCO katika kutambua umuhimu wa radio za jamii.
“Ikiwa wamiliki wa redio watazingatia kutoa maudhui sahihi kwa jamii basi jamii husika itakuwa imejengwa katika msingi ulioimara na dhabiti kwa ajili ya kuleta maendeleo na maelewano,” alisema Prof. Gabriel.
Prof. Gabriel aliongeza kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau katika kuhakikisha kuwa sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji zinazotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) zinafuatwa ili kuepuka msuguano baina ya wamiliki wa radio na serikali.
Vilevile alibainisha kuwa radio ni chombo muhimu sana kwa kuwa kinawafikia watu wengi kutokana na kukua kwa teknolojia ambapo watu wanaweza kusikiliza radio popote wanapokuwa kwa kutumia simu zao za mkononi, tofauti na vyombo vingine vya habari.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Bi. Eda Sanga anaeleza kuwa kwa sasa vipindi vingi vya radio vina maudhui hafifu tofauti na zamani.
“Maudhui ni kitu muhimu sana kwa kuwa kupitia maudhui watu wanapata taarifa na kuelimika lakini zama hizi vipindi vingi vina maudhui ya muziki zaidi kuliko kuelimisha umma” alisema Bi. Sanga.
Bi.Sanga amewataka waandaji wa vipindi kujikita zaidi katika kuandaa vipindi vyenye maudhui muhimu kwa kufanya utafiti wa kina na kuangalia matokeo ya vipindi kwa jamii husika.