Hayo yametolewa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Injinia Joseph Nyamhanga wakati wa mahafali ya 11 ya chuo hicho. Eng. Nyamhanga alichukua fursa hiyo akimwalisha Waziri wa wizara hiyo Makame Mbarawa ambaye alikuwa katika majukumu mengine ya kiserikali.
Katika mahafali hayo, Eng. Nyamhanga hakusita kuutaka uongozi wa chuo hicho kuhakikisha wanatunza vema vifaa vya kufundishia ili vidumu kwa kipindi kirefu ili ziendelee kutoa huduma ya mafunzo kwa wanafunzi wengine waliopo na watakaojiunga na chuo hicho kwa fani mbalimbali za ubaharia.
Aliongeza kuwa kwa sasa Wizara hiyo inajipanga kwa ajili ya utanuzi wa majengo ya chuo hicho kwa ajili ya kutoa fursa kupunguza changamoto ya ufinyu wa madarasa kutokana na ongezeko la wanafunzi. Aliongeza kuwa licha ya kuwa katika mchakato huo, eneo la chuo lililoko Mkuranga nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam tayari wakazi husika waliokuwa wakimiliki eneo hilo wameshalipwa kwa asilimia 98 hali inayotoa fursa kwa chuo hiyo kujipanga zaidi kuboresha mahitaji ya chuo hicho.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho, Meja Jenerali mstaafu Ligata Sande alisema kuwa chuo kinajipanga kuweka mifumo makini kwa ajili ya maendeleo yanayohitajika sanjari na kutoa wahitimu wenye sifa stahiki watakaoweza kupambana na soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Pia msoma risala kwa upande wahitimu Amani Mshana, alisema wanafunzi wa DMI wanakabiliwa na changamoto ya kutoshirikishwa kwa katika vikao vya bodi kutokana na kukosekana kwa mwakilishi hali ambayo inasababisha wanafunzi kushindwa kuwasilisha matatizo yao kwenye bodi ya usimamizi wa chuo na kushindikana kutotekelezwa kwa mahitaji yao.
Aliongeza kuwa chuo hicho kina upungufu wa walimu ambapo kwa sasa mwalimu mmoja anafundisha masomo zaidi ya manne na baadhi yao hawana sifa stahiki hususan katika shahada ya kwanza ya uhandisi wa meli na unahodha. Kutokana na changamoto hizo injinia Nyamuhanga aliwahakikishia wahitimu hao, changamoto hizo kuzifikisha kwa Waziri kwa ajili ya utatuzi.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO.