Katibu Mkuu Kiongozi aapishwa na Rais Kikwete Ikulu

Rais Jakaya Kikwete, akimuapisha rasmi, Balozi Ombeni Yohana Sefue, kuwa Katibu Mkuu Kiongozi badala ya Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Phillemon Luhanjo, aliyemaliza muda wake. Hafla hiyo ya kumuapisha Balozi Sefue, Ikulu Dar es Salaam. Wa pili (kushoto) kwa Rais ni Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Phllemon Luhanjo, akisimamia zoezi hilo. Picha na Muhidin Sufiani-OMR

RAIS wa Tanzania akimuapisha Katibu Mkuu Kiongozi Mpya, Balozi Ombeni Sefue kushikilia nafasi hiyo. Kuapishwa kwa Balozi Sefue ni kunakamilisha kazi ya Rais Jakaya Kikwete alioifanya juzi baada ya kumteua kiongozi huyo mkuu Ikulu.

Balozi Sefue anashika nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo anayemaliza muda wake Desemba 31, 2011. Wasifu wa Balozi Sefue ni mwanataaluma ya diplomasia ambaye tokea Agosti 31, 2010 amekuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.

Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Phillemon Luhanjo (kushoto) akimkabidhi nyaraka za serikali maalum kwa kuapishiwa na Biblia, Katibu Mkuu Kiongozi mpya, Balozi Ombeni Yohana Sefue, ili kuanza kuapishwa rasmi na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu Dar es Salam. Picha na Muhidin Sufiani-OMR


Kabla ya kuteuliwa kwenda Umoja wa Mataifa, Balozi Sefue alikuwa Balozi wa Tanzania katika Marekani mjini Washington DC tokea Juni 15, 2007. Na kabla ya hapo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada nafasi aliyoishikilia kati ya Oktoba 2005 hadi Juni 2007.

Balozi Sefue amekuwa mtumishi wa Serikali tokea 1977 alipoajiriwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwa Ofisa wa Mambo ya Nje. Alipanda nafasi Serikalini na kati ya mwaka 1987 na 1992 Bw. Sefue alikuwa Ofisa Mwandamizi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden Mjini Stockholm.

Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Katibu Mkuu Kiongozi mpya, Balozi Ombeni Yohana Sefue, wakipiga picha ya pamoja baada ya hafla ya kuapishwa rasmi kwa katibu huyo Ikulu Dar es Salaam. Picha na Muhidin Sufiani-OMR


Kati ya mwaka 1993 na 2005, Sefue alikuwa mwandishi wa hotuba na msaidizi binafsi wa marais wawili – Rais Ali Hassan Mwinyi (1993-1995) na Rais Benjamin William Mkapa (1995-2005).

Miongoni mwa mambo mengine, Balozi Sefue alimsaidia Rais Mkapa wakati Rais alipokuwa Kamishna wa Afrika (Kwenye Kamisheni ya Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo –Tony Blair) ambayo ilitoa ripoti iitwayo, Our Common Interest: Report of the Commission for Africa mwezi Machi mwaka 2005, na alishiriki naye kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za G8 ambao ulijadili ripoti hiyo na uliofanyika Gleneagles, Scotland mwezi Julai mwaka 2005.

Rais Jakaya Kikwete, akizungumza na Katibu Mkuu Kiongozi mpya (mteule) kabla ya kuapishwa Ikulu. Kulia ni Phillemon Luhanjo, aliyekuwa akishikilia wadhifa huo. Picha na Ikulu.


Balozi Sefue pia alifanya kazi na Rais Mkapa wakati Mheshimiwa Mkapa alipokuwa Mwenyekiti Mwenza wa Kamisheni ya Shirika la Kazi Duniani ya ILO World Commission iliyojadili Masuala ya Kijamii ya Utandawazi kati ya mwaka 2002 na 2004 ambako alishiriki katika maandalizi ya ripoti ya kamisheni hiyo iitwayo A Fair Globalisation: Creating Opportunities For All, iliyotolewa mwezi Februari mwaka 2004.

Balozi Sefue alipata elimu yake ya juu katika Chuo cha Mzumbe (ambacho kwa sasa ni Chuo Kikuu cha Mzumbe) katika masuala ya Utawala mwaka 1977. Alipata Shahada ya Uzamili katika masuala ya Sera na Utawala kutoka Institute of Social Studies (ISS) mjini The Hague, Uholanzi mwaka 1981.

Pia alipata diploma ya juu katika masuala ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia kutoka Chuo cha Diplomasia cha Dar es Salaam mwaka 1986. Balozi Sefue amemwoa Mama Anita M. Sefue na wana watoto wawili.