KATIBU Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahaman Kinana anatarajia kuanza ziara ya siku 22 kwenye mikoa ya Ruvuma na Mbeya kuanzia tarehe 15/11/2013 mpaka mwanzoni mwa mwezi wa Desemba 2013. Huu ni mwendelezo wa ziara za kichama katika kuimarisha chama, kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kushirikiana nao kuzitafutia ufumbuzi.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Moses Nnauye, amesema katika ziara zilizopita na vikao kadhaa vya chama Serikali iliagizwa kushughulikia baadhi ya kero, hali ambayo baadhi ya hoja hizo zimefanyiwa.
Nnauye alizitaja baadhi ya hoja zilizoanza kushughulikiwa na Serikali ni pamoja na Hoja ya kufufua viwanda nchini. Alisema baada ya ziara kadhaa za Katibu Mkuu, uchambuzi na vikao kadhaa vya CCM, Chama kiligundua kuwa viwanda vingi vilivyo binafsishwa havifanyi kazi kama ilivyokusudiwa na vingine kufungwa kabisa na kugeuzwa magodauni.
“Pamoja na athari kubwa kwa uchumi wa nchi yetu, kufungwa na kutofanya vizuri kwa viwanda hivyo kumechangia sana tatizo la ajira nchini kuwa kubwa. Hivyo Chama kiliagiza Serikali kufanya tathmini ya viwanda vyote vilivyo binafsishwa na hali yake kwa sasa na vile visivyofanya kazi kama ilivyokusudiwa vichukuliwe na Serikali na kutafuta njia sahihi ya kuvifufua upya.” Alisema Nnauye.
Alisema Serikali imechukua hatua kadhaa katika hili, ikiwemo kufanya tathmini na mapendekezo kadhaa yamewasilishwa na timu iliyoundwa na Serikali kwa ajili ya kufanyia uamuzi na kuchukua hatua.
Aidha alisema changamoto kwa wakulima wa pamba baada ya ziara ya Katibu Mkuu wa CCM mikoa kadhaa ya Kanda ya Ziwa, ilichukuliwa na sasa hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vya kutengeneza nyuzi, nguo na kukamua mafuta ya pamba.
“Tulishuhudia ujenzi wa viwanda kadhaa mjini Shinyanga, vingi vikijengwa na wawekezaji kutoka China.
Lakini wakati wa Bunge la juzi, Serikali imeamua kutoa ruzuku ya asilimia hamsini kwa mbegu bora za pamba ili kuwawezesha wakulima kumudu bei ya mbegu hizo na hivyo kuboresha zao la pamba nchini na maisha ya wakulima kuwa bora zaidi.(bei ya dukani kwa kilo moja ni Sh. 1,200/=; Serikali italipia
Sh.600/=).”
“…Katika hili la mbegu bora na kilimo cha mkataba tunaitaka Serikali na hasa wakuu wa wilaya na mkoa kuacha mara moja kutumia nguvu kuwalazimisha wakulima kulima kwa mkataba na kutumia mbegu bora badala yake wawaelimishe na kuwashawishi badala ya kutumia nguvu. Tunaipongeza Serikali kwa kuanza kuchukua hatua za kutekeleza baadhi ya mapendekezo ya CCM ya namna ya kutatua matatizo yanayowakabili wakulima wa pamba nchini. Tunaitaka Serikali kuongeza kasi ya utatuaji wa changamoto hizo ili wakulima wa pamba wafaidike na uchumi wa nchi kukua kwa kasi nzuri,” alisema Nnauye.
Masuala mengine ambayo pia ameyatolea ufafanuzi ni pamoja na migogoro kati ya wakulima, wafugaji na hifadhi juu ya matumizi ya ardhi, ambapo katika ziara mbalimbali za Katibu Mkuu kwenye mikoa kama ya Morogoro, Njombe, Simiyu, Mara n.k. alishuhudia migogoro mingi juu ya wakulima, wafugaji na hifadhi mbalimbali nchini. Alisema migogoro hiyo imegharimu maisha ya watu na mali zao na hata uchumi wa nchi yetu.
“Chama kiliagiza migogoro hiyo kushughulikiwa mapema na kupata ufumbuzi wa kudumu. Chama kinalipongeza Bunge na hasa Wabunge wa CCM na Serikali yake kwa uamuzi wa kuunda Kamati teule ya Bunge kuchunguza na kutoa mapendekezo ya hatua kadhaa za kuchukuliwa katika kufikia suluhisho la kudumu kwa migogoro hii.”
“Tunawaomba wananchi watoe ushirikiano wa kutosha kwa kamati teule ya Bunge ili kazi hii ya kamati iwe na matokeo mazuri yatakayosaidia kumaliza tatizo hili nchini. Wakati Kamati teule ya Bunge ikifanya kazi yake, tunawaomba wakulima na wafugaji kote nchini kutulia kusubiri matokeo ya kamati hii teule ya Bunge,” alisema Nape.
Hata hivyo aliongeza kuwa ziara ya Katibu Mkuu imelenga pamoja na mambo mengine kuimarisha Chama, kukagua Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kusikiliza kero za wananchi, hivyo anaamini ziara hii pia itakua na matokeo mazuri.