WAZIRI wa Katiba na Sheria, Mathias Chakawe amesema upo uwezekazo wa Katiba Mpya ya Tanzania Bara ikapatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Chikawe alizungumza Dar es Salaam jana kuwa, ikiwa mchakato wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano utakamilika kama inavyokusudiwa na rasimu hiyo kupitishwa na wananchi katika ngazi zote bila mabadiliko, muda utakaobaki utatosha kuandaa Katiba ya Tanzania Bara.
“Watu wasiwe na hofu. Sioni tatizo endapo rasimu itapita bila mabadiliko na kupata Katiba Mpya. Aprili mwakani mpaka Desemba inatosha kabisa kuandaa Katiba ya Tanzania Bara na tukaenda katika Uchaguzi Mkuu tukiwa na Katiba Mpya,” alisema na kuongeza:
“Tunaweza kuwatumia wajumbe walewale wa Tume ya Katiba, lakini safari hii tukawachukua wale wa Tanzania Bara pekee wakashiriki katika kuandaa Katiba hiyo.”
Hata hivyo, Waziri Chikawe alisema kutokana na muda kuwa mfupi, Tume hiyo inaweza isifanye kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi kama ilivyofanya sasa na badala yake ikaandaa rasimu na kujadiliwa na wadau kisha kupelekwa katika mabaraza ya Katiba kabla ya kupata Katiba Mpya.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kukamilika Aprili mwakani.
Chikawe anasema kuanzia hapo Serikali inaweza kuitumia tume ya sasa kutangaza rasimu ya kwanza ya Katiba ya Tanzania Bara kwa kurejea maoni iliyokusanya hivyo hatua ya kwanza ikawa ni kujadiliwa kwa rasimu hiyo kwenye mabaraza ya Katiba kwa miezi miwili na baadaye kupelekwa katika Bunge la Katiba jambo litakaloifanya ipatikane mapema.
Waziri Chikawe alisema kinachotakiwa sasa ni kujiandaa kwa Tanzania Bara kuwa na Katiba yake ambayo itatumika kwa ajili ya mambo mbalimbali, ukiwamo Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Waziri huyo aliwatoa hofu Watanzania kwamba hakuna mpango wa kumwongezea muda wa uongozi, Rais Jakaya Kikwete kama ambavyo imekuwa ikielezwa kwani Serikali ina uhakika kwamba kila kitu kitafanyika katika muda uliopangwa.
Siku chache zilizopita Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba alikaririwa akisema kuwa Serikali ina mpango wa kumwongezea Rais Kikwete muda wa kuongoza.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
Wakati Chikawe akitoa kauli hiyo, habari kutoka ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), zinasema kutokana na mapendekezo ya kuwapo kwa Serikali tatu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema anaandaa “kitu muhimu” ambacho atakiwasilisha bungeni siku chache zijazo.
CHANZO: Gazeti Mwananchi