CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeunda kamati ndogo ya watu sita kwa ajili ya kwenda kuonana na Rais Jakaya Kikwete kuwasilisha madai yake juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011, uliopitishwa bungeni juma lililopita.
Kamati hiyo imeundwa katika mkutano wa dharura wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, uliofanyika Dar es Salaam juzi ili kukutana na Rais Kikwete kumjulisha kile walichoeleza kuwa upungufu wa muswada huo na kisha kumtaka atafakari kama ausaini kuwa sheria au la.
Akisoma tamko hilo kwa vyombo vya habari katika mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Chadema jana, Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe alisema kamati hiyo ya watu sita, inafanya taratibu za kumuona Rais Kikwete wakati wowote kuanzia sasa.
Mbowe alisema kamati hiyo itaongozwa na yeye, Katibu Mkuu Dk Willbrod Slaa, Makamu Mwenyekiti (Bara) Said Arfi na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Said Issa Mohamed. Wengine ni Mshauri wa Masuala ya Siasa wa chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Abdallah Safari na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye pia atakuwa katibu wa kamati hiyo wakati wa mkutano huo.
“Hivi sasa taratibu za kumuona Rais zinaendelea, tutamuona wakati wowote kuanzia sasa na kumweleza mapendekezo yetu juu ya upungufu uliomo kwenye muswada wa sheria hiyo na kama atatusikiliza tutashirikiana naye akikataa tutawaeleza wananchi hatua za kuchukua,” alisema Mbowe.
Alisema ushiriki wa Chadema katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya utategemea mazungumzo hayo akisema hiyo ndiyo fursa pekee inayoweza kutumika licha ya muswada huo kupitishwa ‘kibabe’.
“Bado kuna fursa za kisiasa na kijamii katika kujenga mwafaka wa kitaifa juu ya haja ya nia na mchakato na misingi ya Katiba Mpya, Kamati Kuu imesikitishwa na uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete badala ya kuzitumia fursa hizo amejiingiza kwenye upotoshaji uliofanywa na wabunge wa chama chake juu ya misingi na maudhui ya sheria hiyo,” alisema Mbowe na kuongeza,
“Kamati Kuu inaamini badala ya kuwaunganisha Watanzania na kujenga muafaka wa kitaifa unaohitajika katika kuandika Katiba Mpya, hotuba ya Rais Kikwete kwa wazee wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam imezidi kuwagawa wa Tanzania kwa misingi ya ushabiki wa vyama vya siasa kitendo hiki ni hatari kwa Taifa.”
Alisema Katiba si mali ya viongozi wala wanasiasa, bali ni ya wananchi inayohitaji mchango mpana wa maoni yao juu ya kuunda sheria itakayokusanya maoni na hata kuundikwa kwake.
Alisema Chadema kitaendelea kuwaelimisha wananchi na wadau wote juu ya ubovu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na umuhimu wa kuwa na sheria bora itakayoratibu uundwaji wa tume ya kukusanya maoni.
Chama hicho kimewaagiza wabunge na viongozi wake kufanya mikutano ya ndani na ya hadhara yenye lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya sheria hiyo na madhara yake.
Yalia na Polisi
Kamati Kuu ya Chadema pia imelaani kitendo cha Serikali kukizuia chama hicho kufanya mikutano na maandamano nchi nzima kwa kile ilichodai ni kukinyima haki ya kikatiba ya kufanya shughuli zake.
“Polisi kuzuia mikutano ya hadhara ya Chadema na maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga mchakato uliopitishwa kuwa sheria siyo tu kwenda kinyume na haki za msingi za kikatiba, bali pia unahatarisha amani na utulivu wa nchi,” alisema Mbowe.
Aliitaka Serikali kutoa tamko la kufuta amri hiyo huku akisisitiza kuwa Chadema kitaendelea kutumia njia zote za amani zilizopo ikiwemo mikutano ya hadhara na maandamano kama ilivyoainishwa katika Katiba ya sasa.
Kwa nini waligoma?
Awali, Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alitaja sababu saba zilizowafanywa wasusie mjadala huo ikiwamo kukiukwa kwa Kanuni za Kudumu za Bunge wakati wa uwasilishwaji muswada huo.
Alisema Kamati ya Bunge iliingiliwa kazi zake kwa kuzuiliwa kukusanya maoni katika kanda 10 kama ilivyokuwa imepanga na badala yake maoni yakakusanywa kinyume na utaratibu na kuingizwa kwenye muswada huo. Aliishutumu Serikali akidai kuwa iliingilia mchakato huo kwa kumtumia Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Akizungumzia hatua ya wabunge hao kususa, Dk Slaa alisema kamati ilipongeza hatua hiyo akisema ulikuwa uamuzi wa kijasiri uliowafanywa wasiwe sehemu ya kupitishwa sheria mbovu.
“Kamati Kuu imewapongeza wabunge wa Chadema kwa kususia vikao vya kupitisha sheria hiyo kwani ushiriki wao ungeipa uhalali wa kisiasa na kijamii, sheria ambayo haikuzingatia nia ya haja ya dhati ya kuweka utaratibu wa kisheria utakaoiwezesha nchi yetu kupata Katiba Mpya,” alisema.
Wabunge wa Chadema na wenzao wa NCCR-Mageuzi, walisusia kikao cha Bunge kilichojadili na kupitisha Muswada wa Sheria mpya ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.
CHANZO: Mwananchi