Na Anna NKinda – Maelezo, aliyekuwa Mpanda
WAKAZI wa Katavi wametakiwa kulima kilimo cha kisasa na kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo ili waweze kuvuna mazao mengi zaidi ambayo yatawasaidia kupata chakula cha ziada ambacho kitawafaa wao na kuwasaidia mikoa ya jirani. Wito huo umetolewa jana na Mke Wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wananchi hao waliokusanyika katika uwanja wa ndege wa mjini Mpanda kwa ajili ya kumsalimia.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na MAendeleo (WAMA) alisema kuwa Mkoa Wa katavi ni moja ya mikoa inayotegemewa kwa uzalishaji chakula hapa nchini hivyo basi kama wakulima watalima kilimo cha kisasa wataweza kuzalisha chakula kingi na kupata ziada ya kutosha na hivyo kuisaidia mikoa mingine yenye upungufu wa chakula.
Mama Kikwete pia aliwataka wazazi wa Mkoa huo kusimamia elimu ya watoto wao kwa kuhakikisha kuwa watoto wanaenda shule na kukagua madaftari yao ili pale walipokosea waweze kuwarekebisha.
Kwa upande wa wanafunzi aliwataka kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika masomo yao hadi kufika elimu ya juu kwa kufanya hivyo itawawezesha kushika nafasi za juu za uongozi siku za mbeleni.
“Mkisoma kwa bidii, maarifa na kujituma hakika mtafika mbali, sisi hapa tuliopo mbele yenu ni viongozi jitahidini hizi nafasi mje kuzishika ninyi miaka ijayo ili muongoze kuongoza na ninaamini kati yenu kuna viongozi wazuri”, alisema Mama Kikwete.
Mama Kikwete alipita mjini Mpanda alitokea Mkoa Wa Rukwa ambako alikuwa na ziada ya kikazi ya siku tatu pamoja na kazi zingine alizozifanya pia aliikabidhi hospitali ya Mkoa huo kontena lenye mitambo ya kisasa na vifaa tiba vya afya vyenye thamani ya shilingi milioni mia saba.