Kasi ya Kusambaza Huduma za Umeme na Maji Kuongezwa

20131127-185538.jpg

Rais Jakaya Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake itaongeza kwa kiasi kikubwa kasi ya kusambaza huduma za umeme na maji katika vijiji nchini kwa nia ya kuboresha maisha ya wananchi.

Rais Kikwete amewaambia mamia kwa mamia ya wananchi wakati alipozindua miradi ya maendeleo leo, Jumatano, Novemba 27, 2013, katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi ya siku tano ambayo ameianza katika Mkoa mpya wa Simiyu.

Rais Kikwete ameanza ziara hiyo kwa kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Bariadi-Lamadi kwa kiwango cha lami katika sherehe iliyofanyika katika eneo la Old Maswa katika Wilaya ya Bariadi.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 71.8 itauunganisha Mkoa wa Simiyu na mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na inajengwa na Kampuni ya China Communication Construction ya China kwa gharama ya Sh. Bilioni 67.4, fedha ambazo zinatolewa na Serikali ya Tanzania ambayo tayari imemlipa mkandarasi huyo Sh.Bilioni 21.69.

Barabara hiyo ambayo itakamilika katika miezi 30 ijayo, itakuwa na vituo 24 vya mabasi na ilifanyiwa upembuzi wa kina kwa gharama ya Sh .milioni 710.

Akizungumza kwenye sherehe ya uwekaji jiwe hilo la msingi, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake inatumia fedha nyingi kujenga barabara nchini kwa sababu kama “tunadhani tunaweza kuendelea bila kuunganisha nchi yetu kwa barabara za uhakika na kurahisisha usafiri na usafirishaji, tunajidanganya.”
Amesema kuwa barabara hizo zilitakiwa kujengwa miaka mingi iliyopita, lakini nchi ilichelewa sana kuifanya kazi hiyo.
“Hizi barabara tulitakiwa kuzijenga siku nyingi, lakini hali haikuruhusu. Chukua mfano wa ujenzi wa madaraja makubwa. Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 1969 ulisema kuwa tungejenga madaraja yote makubwa kwenye mito yetu mikubwa yote nchini, yaani Daraja la Kirumi kwenye Mto Mara, Daraja la Kilombero kwenye Mto Kilombero, Daraja la Malagarasi kwenye Mto Malagarasi, Daraja la Kigamboni la Dar es Salaam na Daraja la Rufiji kwenye Mto Rufiji,” amesema Rais na kuongeza:

“Lakini Serikali ya Awamu ya Kwanza ilifanikiwa kujenga daraja moja tu la Kirumi…Mzee Mkapa akajenga Daraja la Rufiji…na sisi tunajenga madaraja matatu – Kigamboni, Kilombero na Malagarasi, ambalo limemalizika sasa. Sasa tusipojenga barabara wakati huu tutalazimika kuzijenga baadaye tena kwa gharama kubwa zaidi na bila barabara nzuri na za uhakika, uchumi hauwezi kupanuka kwa kasi inayostahili.”

Akizindua mradi wa usambazaji umeme vijijini katika Parokia ya Nkololo katika Wilaya ya Bariadi, Rais Kikwete amesema kuwa katika kusambaza huduma za umeme kwa kasi zaidi, Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA), utasambaza umeme katika vijiji 1,600 katika awamu ya kwanza ya kazi hiyo katika muda mfupi.

Rais amesema kuwa usambazaji huo wa umeme wa REA ni tofauti na usambazaji umeme unaofanyika chini ya Miradi ya Shirika la Maendeleo ya Milenia la Marekani na Mradi wa Electricity Five unaogharimiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Chini ya miradi hiyo, vijiji 155 katika Mkoa wa Simiyu peke yake vitasambaziwa umeme, kasi ambayo ilikuwa haijawahi kufikiwa wakati wowote katika historia ya Tanzania.

Kuhusu maji, Rais Kikwete amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja ujao, Serikali yake inatarajia kusambaza huduma ya maji katika vijiji 1,449 katika hatua inayokadiriwa kuwa itawanufaisha watu wapatao milioni saba.
Rais Kikwete anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Simiyu kwa kutembelea wilaya za Itilima na Meatu.

Mkoa wa Simiyu ni moja ya mikoa minne ambayo iliundwa na Rais Kikwete mwaka jana na ina wilaya tano ambazo ni Busega, Bariadi, Maswa, Meatu na Itilima.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.