Kashfa ya Escrow Yawagawa Wabunge Dodoma…!

Mbunge, Tundu Lissu (CHADEMA)

Mbunge, Tundu Lissu (CHADEMA)


TUHUMA za uchotwaji wa fedha kiasi cha bilioni 306 zinazodaiwa kuwa za Serikali katika akaunti ya Tegeta Escrow imewagawa wabunge katika mjadala unaoendelea bungeni wa kuijadili ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyowasilishwa na mapendekezo ya kutaka baadhi ya mawaziri, Waziri Mkuu na Watendaji wengine wawajibishwe.

Mjadala mkali unaoambatana na vituko vya wabunge kuzomeana, kupeana vijembe, kukejeliana na kutuhumiana umeanza bungeni mjini Dodoma huku wabunge wakionekana kugawanyika pande tatu yaani wale wanaopinga mawaziri kuwajibika moja kwa moja na wengine kutetea kuwa hakukuwa na kosa fedha hizo kuchukuliwa kwani hazikuwa za Serikali.

Kundi la tatu ni lile linaotaka mapendekezo ya Kamati ya PAC kuungwa mkono na kumtaka Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Waziri wa Nishati na Madini na Katibu Mkuu wake kuwajibika kwa kuvuliwa nyadhifa zao Serikalini kwa kile kushindwa kutekeleza majukumu yao kiasi cha kufanikisha uchotwaji wa fedha hizo.

Baadhi ya wabunge hasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaamini mapendekezo yaliowasilishwa na Kamati ya PAC yamepangwa na kushinikizwa na wabunge wa upinzani wakitaka kumkomoa Waziri Mkuu na Mawaziri wanaotajwa ili wavuliwe nafasi zao jambo ambalo litawaangusha kisiasa.

Wabunge wachache walioanza kuchangia wamesema hawaoni kosa la kumtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mawaziri wengine kuwajibika kwani suala lililotokea si wizi wa fedha kama ilivyotajwa bali ni watu kulipwa fedha walizokuwa wakidai Tanesco.

Kwa upande wake wabunge wa upinzani walioanza kuchangia, Tundu Lissu (CHADEMA) na David Kafulila (NCCR-Mageuzi) wakichangia waliunga mkono hoja ya kuwajibishwa mawaziri, AG, Waziri Mkuu pamoja na watendaji waliohusika kwani fedha zilizoporwa ni za Serikali na zilipaswa kuchukuliwa kwa kufuata taratibu.

Wabunge hawa walihoji kama fedha zinazodaiwa kuporwa hazikuwa za Serikali ilikuwaje majadiliano na idhini ya kutolewa ifanywe na viongozi wa juu wa Serikali huku zikikaguliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilhali hazikuwa za umma. Walisema kuwa kuna kiasi kikubwa cha kodi kilikwepwa na wahusika waliozikomba fedha hizo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Baadhi ya wabunge wa CCM waliochangia walivitaka vyombo vinavyohusika na kodi TRA kufuatilia kwa waliolipwa ili kudai kodi yao na kuitaka Taasisi ya Takukuru kuwachunguza waliogawiwa fedha hizo ili kubaini kama kulikuwa na hongo na mchezo mchafu zaidi ya kung’ang’ania Waziri Mkuu na viongozi wengine wawajibishwe.

Hata hivyo mjadala bado unaendelea bungeni kuhusiana na sakata hilo…