Na Mwandishi Wetu
MABONDIA Jafet Kaseba wa jijini Dar es Salaam na Alibaba Ramadhan wa Arusha wanategemea kupima afya na uzito kesho Jumamosi ya Desemba 21, 2013 saa nne asubuhi katika Ukumbi wa Friends Corner Hotel ambapo ndipo hapohapo pambano lao litafanyikia siku ya Jumapili Desemba 22, 2013 kuanzia saa kumi jioni.
Pambano hilo lililoandaliwa na Ibrahim Kamwe chini ya BigRight Promotion kwa usimamizi wa PST, pia litakuwa na mapambano mengine tisa ya utangulizi likiwemo la ubingwa wa mkoa kati ya Karage Suba na bondia mkali anaechipukia kwa nguvu Fadhili Awadh (tiger) katika uzito wa wealter[66kgs] pambano la raundi kumi, nao wanategemea kupima hiyo kesho.
Akizungumza na vyombo vya habari mratibu wa pambano hilo Ibrahim Kamwe alisema zaidi ya hayo mapambano ya ubingwa mabondia wanaotegemea kupima ni Mbaruk Heri ambaye atapima kwa ajili ya kuzipiga na Lusekelo Daudi, Issa Omar na Mpepeche na Hassan Kiwale ‘moro best’, Zumba Kukwe na Jacob Maganga, Adam Yahaya na Harman Shekivuli, Jocky Hamis na Mbena Rajab, Ernest Bujiku na Shah Kasim, Shaban Bodykitongoji na Mwinyi Mzengela, shaban Manjoly na Kasim Chuma.
Naye Mtanzania aishie Canada Kareem Kutch atapima na Tata Boy kwa ajili ya pambano la kimataifa la mchezo wa kickboxing la raund tano, mabondia wote wameshawasili Dar es salaam. Alibaba Ramadhan wa Arusha na Jacob Maganga wa Tanga wamefikia katika Hotel ya Valley view wakati Kareem Kutch yupo Durban Hotel Kariakoo, wote wapo tayari kwa mapambano yao.