Na Mwandishi Wetu
MAENEO kadhaa ya Soko la Kimataifa la Kariakoo ambalo ni maarufu jijini Dar es Salaam leo tangu majira ya asubuhi yalikuwa yametapakaa maji ya vinyesi yaliyokuwa yakitoka katika njia ya maji machafu.
Mwandishi wa habari hizi aliyekuwa eneo la tukio ameshuhudia maji hayo yakitoka kwenye baadhi ya chemba za vyoo na kutiririka hovyo, hali iliyokuwa kero kwa wafanyabiashara na baadhi ya wateja waliyokuwa wakitafuta mahitaji yao kutokana na harufu kali ya vinyesi iliyokuwa ikitoka.
Mwandishi wa dev.kisakuzi.com ameshuhudia maji ya vinyesi yakiwa yamezagaa zaidi katika maeneo ya nyuma ya makazi ya askari polisi wa kituo cha Msimbazi, maeneo kadhaa ya mtaa wa Kongo na baadhi ya njia za mitaa inalolizunguka Soko la Kariakoo.
Baada ya maji hayo kutiririka kwa muda mrefu majira ya mchana walifika wafanyakazi wa kampuni ya DAWASCO huku wakiwa na gari maalumu la kuzibulia chemba za maji taka. Hata hivyo walishindwa kuyadhibiti maji hayo na kuendelea kutapakaa huku yakikanyagwa na baadhi ya wapitanjia maeneo hayo jambo ambalo lilikuwa hatari kiafya.
Baadhi ya wapitanjia walisikika wakisema; “Kweli hili jiji (Dar es Salaam) limewashinda viongozi wahusika hivyo kuna haja ya kutafuta watu kutoka nje labda wanaweza kuleta mabadiliko…haiwezekani kila wakati miundombinu ya maji taka ikawa kero namna hii tena kwenye jiji maarufu kama hili.”
Hata hivyo juhudi za dev.kisakuzi.com kuwapata viongozi wa soko kungumzia hali hiyo hazikuzaa matunda hadi mwandishi anaondoka eneo la tukio.