Kanisa lashambuliwa Nigeria

Ramani ya nchi ya Nigeria

MAOFISA wa Polisi nchini Nigeria wamesema kuwa watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki wamewauwa watu watatu katika shambulio walilolifanya kwenye kanisa moja, Mji wa Gombe ulioko Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.

Mchungaji wa kanisa hilo, John Jauro amesema waumini wake walishambuliwa wakiwa wakisali sala za jioni. Mchungaji huyo wa Kanisa la Deeper Life ameongeza kuwa mke wake ni miongoni mwa watu waliouawa.

Amesema katika shambulio hilo waumini wengine 10 walijeruhiwa na genge hilo lililokuwa limejihami katika jimbo la Gombe, Kaskazini Mashariki mwa nchi ya Nigeria.

Bado haijulikana aliyetekeleza shambulio hilo lakini kwa kipindi cha majuma kadhaa yaliyopita, kundi la Kiislamu la Boko Haram, limekuwa likishambulia makanisa nchini humo.

Kundi hilo la Boko Haram ambalo limeharamishwa limewataka wakristo kuondoka kaskazini mwa nchi hiyo. Serikali imetangaza hali ya hatari katika maeneo kadhaa ya Kaskazini mwa Nigeria.

Hapo jana washukiwa wawili wa kundi la Boko Haram walikamatwa, baada ya mwanamme mmoja na mwanawe kuuawa mjini Maiduguri, karibu na jimbo hilo la Gombe.
-BBC