RAIA wa Agentina, Cadinali Jorge Mario Bergoglio (76) amechaguliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa katoliki Duniani. Papa Mario Bergoglio ametangazwa usiku huu baada ya kumalizika kwa kikao cha uchaguzi cha Baraza la Makadinali wa Kanisa Katoliki duniani.
Baba Mtakatifu, amejitokeza kwa mara ya kwanza kuwasalimu mamia ya waumini wa Kanisa Katoliki waliokuwa wamekusanyika eneo la St. Peter Basilica, kumshuhudia kiongozi huyo mkuu wa Wakatoliki na mrithi wa Papa Benedict 16 aliyejiuzulu mwezi uliopita kwa hiyari yake mwenyewe.
Bergoglio, ambaye anakuwa kiongozi wa kwanza kushika nafasi hiyo kutoka America ya Kusini amefanikiwa kushika nafasi hiyo baada ya kupata robo tatu ya kura zote za makadinali katika mchakato wa uchaguzi uliochukua siku mbili kwa baraza la makadinali. Kabla ya uteuzi huo, Bergoglio alikuwa ni Kadinali na Askofu Mkuu wa Buenos Aires.
Mingoni mwa viongozi wengine ambao walikuwa wakitajwa kutwaa nafasi hiyo ni pamoja na Kadinali Peter Kodwo Appiah Turkson, ambaye angechakuliwa angelikuwa Papa wa kwanza kutoka Bara la Afrika. Papa mpya wa Kanisa Katoliki anakabiliwa na changamoto kadhaa katika uongozi wake ikiwemo ya kuibuka makundi yanayotaka mabadiliko ndani ya kanisa huku yakipingwa pamoja na kashfa za nyuma za baadhi ya viongozi wa chini wa kanisa kwa watoto.