Na Shomari Binda
Musoma,
Uanzishwaji wa benki itakayokuwa ikitoa mikopo yenye masharti nafuu na isiyo na riba kubwa kwa vijana imedaiwa kuwa itakuwa ndio suruhisho la kujikomboa na kupata mitaji ya kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuwaondoa katika hali ya utegemezi katika jamii.
Kauli hiyo ilitolewa na mgombea wa nafasi ya Makamo Mwenyekiti wa jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM Taifa (UVCCM) Jackson Kangoye alipokuwa akichukua fomu ya kuomba ridhaa kwa vijana wa Chama hicho katika ofisi za Umoja huo Mkoani Mara.
Alisema hali ambayo imewafikisha vijana katika hali waliyokuwa nayo ni kukosa viongozi ambao wanaangalia mbali katika dhana nzima ya kuwainua katika shughuli za kiuchumi ambazo zitwafanya kujiingizia kipato na kuondokana na hali ya utegemezi ambayo wamekuwa nayo vijana kwa muda mrefu.
Alidai iwapo kutaanzishwa benki ambayo itakuwa ikishughulikia masuala ya vijana itapelekea kutimiza kero zao mbalimbali ikiwemo kuwapa mikopo ambayo itakuwa haina dhamana kubwa itakayowafanya kuanzisha miradi ambayo itawawezesha kuingiza kipato na kuendesha maisha yao.
Alisema Umoja wa Vijana unavyo vitega Uchumi sehemu mbalimbali na iwapo kutakuwa na usimamizi mzuri fedha zake pamoja na fedha ambazo zitatafutwa kwa wahisani mbalimbali zitawezesha kuanzishwa kwa benki ambayo itatekeleza malengo aliyoyakusudia.
“Tunavyo vitega uchumi vingi katika umoja wetu ambavyo tukivitumia vizuri vitatuletea manufaa nakumfanya kila kijana kuishi maisha mazuri kwa kujiingizia kipato kitakachomuwezesha kukabiliana na hali ya maisha,”alisema Kangoye
Aliongeza kuwa kupatikana kwa viongozi ambao watakuwa na maono ya mbali katika kuwaletea mabadiliko vijana ndio kutawafanya kuondokana na hali ya kuwa ombaomba na kutumiwa na viongozi wa kisiasa katika kuwapigia debe na kuwaweka katika nafasi.
Mara baada ya kuchukua fomu Kangoye alisisitiza kuwa iwapo atachaguliwa katika nafasi hiyo ya Makamo Mwenyekiti wa (UVCCM) Taifa atahakikisha kwa kushirikiana na viongozi wengine benki ya Vijana inaanzishwa itakayokuwa na marengo ya kuwanufaisha Vijana.
Tayari mgombea huyo amesharudisha fomu ya kuomba kuchaguliwa na mkutano mkuu wa Umoja huo katika ofisi za Makao Makuu Jijini Dar es salaam na kusubili vikao vya uteuzi na kuingia katika kinyang’ang’a nyiro na vijana wengine walioomba nafasi hiyo.