KAMPUNI ya mawasiliano ya simu ya Halotel, imeipongeza serikali kwa kuweka mfumo wa kukusanya kodi kwa njia rahisi na yenye uwazi na kufafanua kuwa wao wamekuwa kampuni ya kwanza kujiunga na kufurahia utaratibu huo kama ilivyobainishwa na kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere, kwani unawezesha kampuni kuwa wazi katika malipo yote ya kodi na tozo wanazozifanya kwa wateja.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo bwana Le Van Dai, amefafanua kuwa wao kama kampuni siku zote wamejiweka mbele katika kuhakikisha wanatimiza matakwa ya serikali kwa kufuata taratibu zote zinazowekwa na mamlaka husika.
“Tulipofahamishwa kuhusu utaratibu huu wa ukusanyaji kodi tulifurahia sana kwa sababu unaweka wazi maendeleo ya biashara na ukusanyaji wa mapato ya serikali, sisi kama wawekezaji tunafurahia kuwa na njia bora za usimamizi wa mapato ya serikali na kampuni husika kwani unatuwezesha sisi pia kujipima kujua biashara kama ni nzuri au sivyo na kuangalia namna bora ya kushauriana na mamlaka husika katika kufanikisha mazingira bora ya kibiashara” Alisema Dai.
Aidha, Mkurugenzi huyo pia aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wanaendelea kufurahia mafanikio ambayo kampuni hiyo imekuwa ikiyapata tangu kuanzishwa kwake.
“Katika taarifa ya robo ya kwanza ya mwaka huu 2017 iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeonesha namna ambavyo kampuni yetu imeendelea kufanya vyema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita,”
“Kimsingi, idadi ya wateja wa kampuni za simu ilipungua kutoka 40,173,783 kwa Desemba mwaka jana na kufika39,856,212 kwa Machi mwaka huu. Hii ina maana kuwa kuna baadhi ya mitandao ya simu ilipoteza wateja ila Halotel tumeweza kuongeza wateja wapya wapatao 73,872. Hii ni ishara kuwa Watanzania wanaridhika na huduma zetu. Tunawaahidi kuwa hatutawaangusha,” alisema,”
Alisema Dai na kuongeza kuwa “hii ni dalili nzuri kwetu kibiashara. Tunawashukuru Watanzania kwa kuendelea kutuamini na kuendelea kujiunga na sisi, tunawaahidi kuendelea kuboresha huduma zetu na kuufanya Halotel uendelee kuwa Mtandao chaguo namba moja kwao.” Alihitimisha Mkurugenzi huyo.
Pamoja na mambo mengine Mkurugenzi huyo amesema kampuni hiyo bado inatoa kipaumbele kwa kutoa huduma bora kwa jamii ya Watanzania ikiwepo pamoja na kuwezesha miundombinu ya mawasiliano kwa taasisi mbalimbali za serikali pamoja na taasisi za kijamii, zikiwemo shule, hospitali, ofisi za posta na halmashauri mbalimbali. Hivi karibuni kampuni hiyo ilitangaza uwekezaji wa Zaidi ya bilioni 200 katika kuboresha ubora wa mtandao huo, ikilenga kuongeza kasi ya intaneti na ubora wa huduma za sauti.