Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) yadhamini mkutano wa Jukwaa la wahariri Arusha


Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri Tanzania, Absalom Kibanda (wa tatu kushoto) akizungumza na wanahabari leo.

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa kushirikiana na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), wamendaa mkutano wa kitaaluma wa wahariri utakaofanyika Arusha kuanzia Alhamisi, Julai 14 hadi Jumamosi, Julai 17, 2011.

Mkutano huo utawashirikisha wahariri wapatao 80 kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ambapo mada kuu ni “Responsible Journalism” kwa tafsiri isiyo rasmi ni Uandishi wa Habari unaozingatia Wajibu’.

Miongoni mwa mada zitakazowasilishwa na kujadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na hali ya utendaji wa vyombo vya habari, maadili ya waandishi wa habari ndani na nje ya vyumba vya habari, athari za uandishi wa habari unaoegemea upande mmoja, makosa katika utangazaji na uandishi wa habari na wajibu katika habari za michezo.

Mbali na mada hizo, wahariri watapata fursa ya kutembelea kiwanda kipya cha kuzalisha bia kilichopo mjini Moshi. Pia kutakuwa na mchezo wa mpira wa miguu kati ya jukwaa la wahariri na timu ya wafanyakazi wa kampuni ya bia ya Serengeti katika uwanja wa TPC siku ya Jumamosi tarehe 16Julai.

Mbali na hayo, wahariri watashiriki katika tamasha kubwa la muziki la Serengeti Fiesta litakalofanyika Jumamosi katika uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurungenzi wa SBL, Jaji Mark Bomani atatoa Mada ya Ufunguzi kwa wahariri Alhamisi jioni na wahariri wataendelea na mkutano wao wa ndani Ijumaa Julai 15,2011.