Kampeni Igunga: Rostam amtumia Mkapa

 

Rostam Aziz

 

Mwandishi wetu

– Adaiwa kumwangukia ashirikishwe

KAMPENI za uchaguzi mdogo Jimbo la Igunga zinazinduliwa mwishoni mwa wiki huku kukiwa na taarifa kwamba kuna mgawanyiko ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) juu ya ushiriki wa mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Rostam Aziz, Raia Mwema limearifiwa. Taarifa za ndani ya CCM zimethibitisha kwamba chama hicho kilimwomba rais mstaafu Benjamin Mkapa kuongoza kampeni hizo na kwamba hakijapata kutoa mwaliko kwa mwingine, japo taarifa za vyombo vya habari zimekuwa zikisema Mkapa angeungana na Aziz katika shughuli hiyo.

Ni utata huo unaoelezwa sasa kuwa umezua mvutano wa ndani, baadhi wakisema kwamba Aziz hajaalikwa na wengine wakishinikiza kwamba ashiriki hata kama yeye mwenyewe alikwishakutangaza kwamba ameacha kabisa siasa. Wakati Mkapa akifungua kampeni za CCM, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Wilbroad Slaa, atazindua kampeni za CHADEMA na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, atazindua kampeni za CUF.

Taarifa zilizopatikana tukienda mitamboni zinasema zimekuwapo jitihada za kutoka upande wa Aziz za kushawishi timu ya Mkapa imshirikishe kwenye kampeni hizo. Lakini taarifa huru kutoka ndani ya Kamati Kuu ya CCM na watu walio karibu na Rais Jakaya Kikwete zinaeleza kuwa, Kamati Kuu haikuwahi kumwomba rasmi Rostam ashiriki kampeni hizo, hali ambayo imekuwa ikitajwa na watu waliokaribu naye kuwa imekuwa ikimsumbua.

Kwa muda mrefu, Rostam amekuwa akishiriki shughuli mbalimbali za CCM hasa za maandalizi ya uchaguzi na wakati mwingine amekuwa akihusika kwenye kamati za kutafuta fedha, lakini wakati huu, mambo yamekuwa kinyume kwake licha ya kwamba ndiye aliyekuwa Mbunge wa Igunga. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa amewahi hata kushiriki katika baadhi ya mikakati ya kampeni za mwaka 2000 za Benjamin Mkapa, na 2005, kamati ya kampeni za Jakaya Kikwete.

 Taarifa za uhakika kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu walioshiriki kikao cha mwisho cha chombo hicho hivi karibu, pamoja na baadhi ya wasaidizi wa Rais Kikwete, zinaeleza kuwa mbunge huyo wa zamani amekuwa akijitahidi kupata miadi na Kikwete bila mafanikio na ameelekeza matumaini yake kwa Mkapa sasa, ambaye ametangazwa kuongoza kampeni za CCM Igunga. “Hakuna popote kwenye Kamati Kuu ambako Rostam ameombwa kushiriki kampeni za Igunga, tulishangaa kuona baadhi ya magazeti yakiandika hivyo kama vile habari hiyo imeratibiwa kwa taratibu na malengo maalumu. “Tunajua Rostam amekuwa akifanya lobbying (ushawishi) kwa Ndugu Mkapa amshirikishe kwenye kampeni hizo.

Sisi kama chama hatuna tamko rasmi la kikao tukimtaka ashiriki kampeni na kwa kweli chama kitaendelea kusimamia uamuzi wake wa vikao vya awali (Halmashauri Kuu-NEC) ukiwamo wa kujivua gamba,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu, aliyeshiriki kikao kilichomteua Mkapa kuzindua kampeni za CCM. Lakini wakati mjumbe huyo akisema hayo, taarifa zaidi kwa watu waliokaribu na Rais Kikwete, wakiwamo baadhi ya wasaidizi wake, zinaeleza kuwa hakuna siku ambayo Rostam amekutana na Kikwete au Kikwete kutoa maelekezo kuwa Rostam ashiriki kampeni za Igunga, ingawa kumekuwapo na jitihada za kuhamasisha suala hilo kwa njia mbalimbali, ikiwamo kwa kutumia baadhi ya vyombo vya habari. “Imedhihirika kuwa Rostam au watu wake wanaweza kucheza na vyombo vya habari na kujenga dhana yoyote wanayoamini itawasadia kwa mujibu wa mikakati yao, kama hili suala la kusema Kamati Kuu imemtaka aende Igunga ambalo si kweli. “Wengine wanasema eti Rostam ameombwa hata na Rais Kikwete na amekutana naye. Si kweli, Rais hakuwahi kukutana na Rostam na wala hakuna chochote ambacho Rais ameelekeza kuhusu Rostam kwenda Igunga,” alisema mmoja wa watu waliokaribu na Rais Kikwete.

 Taarifa hizo zinaibuka katika wakati ambao tayari baadhi ya vyombo vya habari, takriban wiki mbili zilizopita, vikiwa vimeripoti kuwa Rostam ameombwa rasmi kushiriki kampeni za Igunga, licha ya uamuzi wa awali wa kumtaka ajivue madaraka yote ndani ya CCM, yeye pamoja na wenzake, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge. Kampeni za CCM jimboni Igunga zinatarajiwa kuzinduliwa na Mkapa Jumamosi (Septemba 10, 2011) ambapo atakuwa na jukumu la kumnadi mgombea wa chama hicho jimboni humo, Dk. Dalali Peter Kafumu, ambaye ndiye aliyekuwa Kamishna wa Madini katika Wizara ya Nishati na Madini. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amewahi kuzungumzia suala hilo akikiri kuwa CCM hakikuwahi kutoa mwaliko rasmi kwa Rostam, isipokuwa kwa Mkapa pekee na kwamba, yeyote ambaye ni mwanachama wa chama hicho anaruhusiwa kushiriki kampeni.

Moja ya magazeti yaliyoandika Rostam ameombwa na Kamati Kuu kushiriki kampeni lilimnukuu Nape akisema; “Ukiachilia mbali watu kama Mzee Mkapa ambaye atakuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi, hatukupeleka mwaliko kwa mtu mmoja mmoja, ila tuliwaalika wanachama wetu kusaidia kampeni hizi, kwa hiyo Rostam akiwa mwana CCM ana haki ya kukipigia kampeni chama chake.” Uchaguzi wa Igunga unatarajiwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu, ambako mbali na mgombea huyo wa CCM, wagombea wengine ni pamoja na Moses Edward (TLP), Joseph Kashindye (CHADEMA), John Maguma (SAU) na Leonard Mahona (CUF). CCM kwa sasa imekuwa katika mtihani mkubwa kutoka kwa wananchi baada ya kutangaza uamuzi wake wa kujivua gamba ambao unajumuisha wito wa kuwataka baadhi ya viongozi wake wenye tuhuma ukosefu wa maadili kujiuzulu nyadhifa zote walizonazo ndani ya chama hicho. Msingi wa uamuazi huo ni hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho, aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, yaliyofanyika kitaifa mkoani Dodoma, Uwanja wa Jamhuri. Katika hotuba hiyo, Kikwete alisema chama chake ni lazima kijitazame upya ili kurejesha imani ya wananchi na hasa katika suala la uadilifu wa viongozi wake.

Hotuba hiyo, ilifuatiwa na uamuzi wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, ambacho pamoja na maazimio mengine, kilifanya mabadiliko ya kiuongozi kwa kuiondoa Sekretariati iliyokuwa chini ya Katibu Mkuu, Yusuf Makamba na kuingiza Sekretariati inayoongozwa na Wilson Mukama. Chama hicho pia kiliazimia viongozi wenye madaraka ya utendaji waachie madaraka mengine waliyonayo ndani ya Serikali. Hata hivyo, tangu uamuzi huo ufikiwe wa kujivua gamba, ni Rostam pekee ndiye amejiuzulu nyadhifa zake, huku wenzake, Lowassa na Chenge, wakibaki kimya, ingawa taarifa za hivi karibu zinaeleza kuwa; katika kikao chao na Pius Msekwa, anayesimamia mchakato wa kujivua gamba, Lowassa na Chenge, waliomba muda wa kutafakari zaidi, ingawa mwenzao Rostam aliwahi kuhitimisha tafakari yake na kujiuzulu. Mara mwisho, CCM ilieleza kuwa suala hilo la kujivua gamba litahitimishwa kwenye kikao kijacho cha NEC ambacho kilitajwa kufanyika mwezi huu wa Septemba, wakati ambao kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Igunga zitakuwa zinaendelea kabla ya upigaji kura mwanzoni mwa Oktoba, mwaka huu.

Wakati huohuo, mgombea wa ubunge jimbo la Igunga kwa tiketi ya CCM, Dk. Dalaly Peter Kafumu amerejesha fomu kwa msimamizi wa uchaguzi na kusema anao uhakika wa kutapata ushindi usio na shaka. Akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kurejesha fomu hizo ili kuteuliwa rasmi kuwa mgombea, Dk. Kafumu pia ametaja mikakati yake kuwa ni pamoja na kuifanya Igunga kuwa ya kisasa kimaendeleo. Dk. Kafumu alisema, miongoni mwa atakayoyapa kipaumbele katika kuijenga Igunga ni uboreshaji wa huduma za maji, uboreshaji miundombinu ya barabara hadi vijijini ikiwemo inayounganisha Igunga na Manonga. Aliahidi kusimamia ujenzi wa daraja la Mbutu kwa kusimamia upatikanaji wa fedha za mradi huo ambazo alisema anafahamu kuwa serikali imeshazitenga na kilichobaki ni usimamizi wa fedha hizo kufika Igunga.

Dk. Kafumu alisema, atasimamia kwa karibu kuhakikisha shule zinapata mahitaji muhimu na pia kusimamia uboreshaji wa kilimo cha pamba na ufugaji ili sekta hiyo ifanyike kisasa zaidi jimboni humu. “Baadhi ya mambo haya yameshafanywa kwa kiasi chake na mbunge wetu aliyepita Rostam Aziz, basi nitahakikisha kuanzia pale alipoishia kuyaboresha zaidi na kuanzisha mapya ambayo itaifanya Igunga kupiga hatua ya kupigiwa mfano hapa nchini”, alisema.

Chanzo: RaiaMwema