Kambi ya Stars Yavunjwa Baada ya Chad Kujitoa

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’

TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imevunja kambi na wachezaji wameruhusiwa kurejea kwenye klabu zao.

Tanzania ilikuwa icheze na Chad kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mechi ya Kundi G kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2017 nchini Gabon.

Lakini Chad Jana imejitoa kwa sababu za kiuchumi wakiandika barua Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kusema kwamba hawana fedha za kuwawezesha kuendelea na mechi za Kundi G.

Chad inajitoa baada ya kukamilisha mechi tatu za mzunguko wa kwanza, ikifungwa zote 2-0 na Nigeria ugenini, 5-1 na Misri nyumbani na 1-0 na Tanzania nyumbani Jumatano.

Sasa Kundi G linabaki na timu tatu ambazo ni Tanzania, Nigeria na Misri.
Wenyeji Tanzania wamekuwa kambini hoteli ya Urban Rose, katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwa maandalizi tangu warejee kutoka D’jamena, Chad Alfajiri ya Ijumaa baada ya mchezo wa kwanza walioshinda 1-0 Jumatano iliyopita.

wachezaji waliokuwa kambini Taifa Stars chini ya makocha Charles Boniface Mkwasa na Hemed Morocco kwa maandalizi ya mchezo huo ni makipa; Shaaban Kado (Mwadui FC) Aishi Manula (Azam FC ) na Ally Mustafa ‘Barthez’ (Yanga SC).

Mabeki; Juma Abdul (Yanga SC), Shomary Kapombe, Mwinyi Hajji (Yanga SC), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Kevin Yondan (Yanga SC) na David Mwantika.

Viungo; Ismail Khamis ‘Suma’ (JKU), Said Ndemla (Simba SC), Jonas Mkude (Simba SC), Mwinyi Kazimoto (Simba SC), Himid Mao (Azam FC ), Mohammed Ibrahim (Mtibwa Sugar), Ibrahim Hajib (Simba SC), Deus Kaseke (Yanga SC), Farid Mussa (Azam FC ) na Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar).

Washambuliaji ni John Bocco (Azam FC ), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC), Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji), Elias Maguri (Stand United), Jeremiah Juma (Prisons FC) na Abdillahi Yussuf ‘Adi’ (Mansfield Town, England).

Stars inashika nafasi ya tatu katika Kundi G, kwa pointi yake moja baada ya ufungwa na Misri 3-0 na kutoa sare ya 0-0 na Nigeria.

Misri inaongoza Kundi hilo kwa pointi zake nne, ikifuatiwa na Nigeria yenye pointi mbili. Misri na Nigeria wanarudiana Jumanne Cairo baada ya kutoa sare ya 1-1 Jumapili Kaduna.
Habari Kwa Hisani ya Bin zubery.co.tz