Kamati ya Wanafunzi Ustawi wa Jamii yazungumza na wanahabari Dodoma

JULAI 21, 2011, Taasisi ya Ustawi wa Jamii ilifunga masomo (kufunga Chuo) kutokana na mgogoro baina ya Menejimenti na Wahadhiri. Mgogoro huo ambao Kaimu Mkuu wa Taasisi hiyo, Mlwande Madihi alisema umesababisha mgomo usio halali wa wahadhiri, umekuwa na madhara makubwa kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kukosa malazi na kushindwa kujikimu kimaisha huku wengine muda wao wa ruhusa kazini ukizidi kuisha.

Kutokana na hali hiyo, Julai 21, 2011 Mkutano Mkuu wa Wanafunzi uliunda Kamati Maalumu ya Dharura kwenda Dodoma kuwasilisha kilio cha Wanafunzi kwa Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kueleza madhara ya kufunga Chuo.

Kamati ilifika Dodoma Julai 24, 2011 na Julai 26, 2011, Kamati ikiongozwa na Kaimu Mwenyekiti Chrisanti Mutatina, Makamu Mwenyekiti, Mariam Saad na Katibu, Safari Kitamogwa, ilionana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na kisha Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya. Siku iliyofuata Kamati hiyo ikiwa na Wajumbe 10 ilikaribishwa katika kikao cha Bunge. Wajumbe hao ni Benezeth Boniphace, Julieth Muchunguzi, Joseph Sabinus, Godfrey Kinogo, Johnson Rutechula, Machibya Mayala na Khadija Mkwama.

Kamati pia ilifanikiwa kuwasilisha kilio chake Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi Dodoma na kuonana na Viongozi wafuatao:

(1) Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (MB), Katibu wa NEC wa Uchumi na Fedha

(2) Ndugu Martin Shigella, Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kitaifa

(3) Ndugu Nape Nnauye, Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi

Alhamisi Julai 28, 2011, Kamati ilionana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Hussein Mponda.

Awali katika mazungumzo yetu ofisini kwake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Kawambwa alisema watakutana na Waziri wa Afya kujadili na kutoa suluhisho la kudumu kwa tatizo la Chuo cha Ustawi wa Jamii, na pia akaahidi kushughulikia ombi la wanafunzi kuwa Chuo kifunguliwe mapema. Aliwasihi wanafunzi wawe wavumilivu na waendelee kujisomea wakati Serikali ikishughulikia suala hilo mapema iwezekanavyo.

Naye Dk. Nkya aliwaambia Wanakamati kuwa wawe watulivu kwa kuwa Serikali inashughulikia suala lao. Kwa upande wake, Waziri Mponda (Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii) alisema, tatizo tayari linafahamika na Serikali inaguswa na matatizo ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii na hivyo kuahidi kulishughulikia haraka.

Mhe. Mwigulu Nchemba (Mb) alimwambia Waziri Mponda katika mazungumzo hayo na Wanakamati ndani ya ofisi za Bunge kwa kuwa mgomo haukuwa wa wanafunzi na hawakuwahi kuwa sehemu ya mgogoro, Chuo kitakapofunguliwa ni vyema wanafunzi wote warudishwe chuoni bila masharti wakiwamo wanakamati wote.

Katika hoja hiyo, Waziri Mponda amesema wanafunzi hao kwa vyovyote sio sehemu ya mgogoro, bali ni waathirika na hivyo Serikali iko makini kuhusu usalama wao ukiwamo wa kimasomo.

Wanakamati walimweleza Waziri kuwa, baadhi ya watu wamejaribu kupotosha wakisema wanafunzi waligoma ingawa ukweli ni kwamba walifanya Mkutano Mkuu halali ulioitishwa na Rais wa Serikali ya Wanafunzi (ISWOSO), Gerlad Julio Simbeya na kuahidiwa kupatiwa majibu siku iliyofuata toka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa Taasisi.

Ndipo katika hali ya kushangaza wakatangaziwa kuwa Chuo kimefungwa kwa muda usiojulikana kutokana na mgomo usio halali wa wahadhiri na kutakiwa kuondoka Chuoni mara moja.

Kamati hiyo imependekeza kwa Waziri Mponda kuwa Serikali iwarudidshe kazini wahadhiri waliogoma ili masomo yaendelee na kama kuna tatizo hatua zichuliwe kwa wahusika wakati wa likizo ya takriban miezi mitatu ikiwa ni pamoja na kuajiri wahadhiri wengine

Viongozi hao wa CCM walisema, umefika wakati vyombo vya Serikali kufanyia kazi chanzo cha migogoro badala ya kushughulikia matokeo ya migogoro.

Aidha, Ndugu Shigella, Katibu wa Vijana wa CCM aliahidi kufikisha matakwa ya vijana wenzake katika ngazi na mamlaka husika.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kinondoni (CCM) Idd Azzan, alimwambia Waziri Mponda kuwa Serikali haina budi kushughulikia haraka kero zilizopo katika Taasisi hiyo kwa wakati ili wanafunzi wamalize muhula wa masomo kwa wakati kwani wao sio sehemu ya mgogoro.

Waziri alisema Serikali inaangalia namna ya kuwasaidia wanafunzi kwa muda utakaoongezeka.

Hivyo, kwa kauli hizo, Kamati hii inapenda kuutangazia umma kuwa Serikali imeyapokea vizuri maombi ya Kamati hiyo na pia inakipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mawaziri hao kutokana na ushirikiano na ukarimu walioionyesha Kamati hiyo.

Katika hatua nyingine, Kamati imesikitishwa na taarifa iliyomnukuu Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Dodoma , Stephen Zelothe ikisema Wajumbe wanane wa Kamati hiyo wote wakiwa wa jinsi tofauti, wamekamatwa na Polisi kwa tuhuma za kukutwa katika chumba kimoja ndani ya nyumba ya kulala wageni iitwayo Vatican .

Kamati imeshangazwa na taarifa ya Kamanda Zelothe kuwa Wajumbe wote walilala chumba kimoja ilihali akijua Wajumbe hao wa Kamati walikamatwa kwa tuhuma za kutojiandikisha katika Daftari la Wageni kwani ni mmoja kati yao aliyejiandikisha kwa niaba ya wengine na kutaja idadi ya vyumba vitano.

Tunaomba umma pamoja na RPC Zelothe kutambua kuwa taarifa hiyo potofu imetuumiza kisaikolojia na kutikisa mahusiano yetu na familia zetu. Aidha, tunamuomba Kamanda Zelothe kutoa taarifa sahihi kwa vyombo vya habari ili kulinda heshima ya Jeshi la Polisi mkoani humo. Huo ndio ukweli na hiyo ndiyo hali halisi iliyojiri.

Ahsanteni.

…………………………………. …………………………………..

CHRISANT MUTATINA MARIAM SAAD

KAIMU MWENYEKITI MAKAMU MWENYEKITI

0717 745030 0717 510851

………………………………

KITAMOGWA SAFARI

KATIBU

0716 760951 / 0763 432292