Coastal Union imepoteza mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga baada ya washabiki wake kuwa chanzo cha Mwamuzi kuvunja mchezo huo uliofanyika Aprili 24, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana leo (Aprili 27, 2016) jijini Dar es Salaam kwa kuzingatia Kanuni ya 28(2) ya Kombe la Shirikisho. Wakati mechi hiyo inavunjwa, Yanga ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-1.
Pia Coastal Union imepigwa faini ya sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kuzingatia Kanuni ya 42(26) ya Ligi Kuu kutokana na vitendo vya vurugu za washabiki wake wakati wa mechi hiyo. Pia TFF haitasita kufungiwa uwanja huo iwapo vitendo hivyo vya vurugu za washabiki havitakoma.
Mwamuzi wa mchezo huo Abdallah Kambuzi amefungiwa mwaka mmoja wakati Mwamuzi Msaidizi namba mbili Charles Simon ameondolewa kwenye ratiba ya waamuzi. Adhabu hizo zimetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1) ya Ligi Kuu.
Mchezaji Adeyum Ahmed wa Coastal Union anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi kutokana na kitendo chake cha kumpiga kichwa Mwamuzi wa Akiba baada ya kutolewa nje. Hata hivyo, Ahmed hakufanikiwa kutimiza azma hiyo baada ya Mwamuzi huyo kumkwepa.
Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kutokana na kutoingia vyumbani kwenye mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho.
Vilevile malalamiko ya Coastal Union kutaka mechi hiyo irudiwe yametupwa baada ya Kamati ya Mashindano kubaini kuwa hayana msingi wowote.